WANANCHI wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanakabiliwa na magonjwa ya upumuaji, kuharisha magonjwa ya ngozi kutokana na hali halisi ya uchafu na moshi unaotoka ndani ya maboma ya wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Zahanati ya Oloirobi Tarafa ya Ngorongoro Kata ya Ngorongoro, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Silvia Malloy alisema wagonjwa wengi wanaofika kupatawa matibabu wanatokana na magonjwa hayo matatu yanayosumbua zaidi.
Alisema sababu kubwa ya magonjwa hayo yanachangiwa na hali halisi ya mazingira ya baridi na jamii hiyo kushindwa kujisitiri nyakati za baridi hasa ugonjwa wa niomonia na mazingira ya usafi wa chakula si mazuri pamoja na magonjwa ya ngozi sababu wanalala na mifugo kama mbwa ndani ya maboma yao.
“Nyumba wanazoishi zinasababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji sababu wanakoka moto ndani yake na kulala na mifugo ndani, lakini pia maboma yao hayana madirisha ya kutolewa hewa hali inayofanya ndani kuwa na moshi mkubwa unaoleta madhara kwao,” alisema.
Zahanati hiyo inahudumia vijiji vitatu ambavyo ni Oloirobi, Kayapus na Mokilal ambapo awali msanii Suleiman Msindi maarufu kwa jina la” Afande Sele” alitoa rai kwa wananchi hao kuhama kwa hiyari kwani mazingira halisi ya maboma yao kwa baadhi ya jamii hiyo ya kifugaji si rafiki kutokana na kuishi na mifugo ndani ya boma.
Aliisisitiza kuwa ni vema sasa wananchi hao wakahama katika hifadhi hiyo na kwenda kuishi kwenye mazingira bora ambayo nyumba za huko zina madirisha rafiki kwa maisha ya binadamu ikiwemo huduma zote za kijamii.
Naye mmoja kati ya wananchi hao alizungumzia kuhama, Naskoi Ndarakwai aliiomba serikali kuwaondoa haraka kwani wanapoumwa vifua wanakumbana na changamoto mbalimbali sababu ya hali halisi ya mazingira kwani maboma hayo kwa ndani yana joto sana na moshi unaowaletea athari za kiafya.