Daktari: Pombe zinaua seli za ubongo

DAKTARI bingwa bobezi wa magonjwa ya mfumo wa fahamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk Mohamed Mnacho amesema matumizi ya pombe yaliyopitiliza yanaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa fahamu kwani kemikali zilizopo kwenye pombe zina tabia ya kuleta madhara kwenye seli za mfumo wa balansi ya ubongo.
Daktari Mnacha ameshauri kuwa ni vema kama mtu anahitaji kunywa pombe akatumia si zaidi ya chupa moja kwa siku ili kuendelea kujikinga na magonjwa yanayoathiri mfumo wa fahamu. Dk Mnacho amesema baada ya uharibifu seli za ubongo zinaweza kufa kabisa.
Ameeleza kuwa mtu akinywa pombe na kulewa maana yake anakuwa ameathiri mfumo wa balansi ya ubongo hivyo akiendelea na tabia hiyo mara kwa mara seli za ubongo zitakufa.

Dk Mnacho amebainisha kuwa mtu aliyeathirika na changamoto za mfumo wa balansi za mfumo wa ubongo ataanza kupata changamoto za kusahau, kutetemeka, kuchanganyikiwa na baadaye anaweza kupata kifafa ambacho kitampelekea kutumia dawa za kifafa kila siku.
“Ni vizuri jamii ikajiepusha na matumizi ya pombe yaliyokithiri kwa kuwa pombe ikizidi inakuwa ni sumu na madhara yake ni ya muda mrefu.
SOMA: Pombe haramu yaua 34 India
Amefafanua kuwa endapo mtu akipata magonjwa haya yatokayo na athari ya matumizi ya pombe matibabu yake yana gharama kubwa na yanatumia muda mrefu kuyatibu.



