MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dk. Rashid Mfaume ametangaza mkakati wa mkoa kudhibiti ugonjwa wa Marburg ambao upo mkoani Kagera.
Akizungumza na HabariLeo, Dk Mfaume amesema mashine za utambuzi wa magonjwa ya mlipuko ikiwemo Covid 19, Ebola zilizokuwa zimefungwa uwanja Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kwa wasafiri wa nje zimehamishwa na kuweka kwenye uwanja wa zamani ambao unatumiwa na wasafiri wa ndani.
Amesema wamefanya hivyo kutokana na muingiliano mkubwa uliopo kutokana na ndege zinazotua kila siku kutoka Kagera au nyingine kupitia Kagera na mikoa ya jirani kama Mwanza na Kigoma
Amesema pia wamefunga mashine za utambuzi wa magonjwa katika kituo cha Magufuli Mbezi Luis ambapo pia mabasi yote kuna wataalamu ambao wanakua na fomu ambazo zinajazwa na kuwa na ufuatilia kwa abiri wote wanaoingia hususani kutoka mikoa ya Kagera na mikoa ya jirani.
“Ufuatialiji hatuangalii tu dalili, hata waliochangamana na watu, lengo ni kuhakikisha ugonjwa wa marburg hauingii Dar es Salaam.”Amesema.
Hata hivyo Dk Mfaume amesema jukumu la kwanza la kujilinda ni la mwananchi mwenyewe kuepuka kuchangamana kwenye misongamano isiyo ya lazima kufuatia milipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC Kongo, Kipindupindu Malawi na Marburg Kagera.
“Wafanyabiashara Kariakoo wengi wanatoka Kongo, jukumu la kwanza ni mwananchi mwenyewe, wafuate zile njia ambazo wameelekezwa za kujikinga, kuepuka msongamano, kuepuka kusalimia kwa kushikana mikono, kukumbatiana, kunawa mikono na maji tiririka na sabuni, kuepuka kuhudhuria mazishi ya mtu ambaye kifo chake sababu zake hazijulikani” Amesema
Marburg, Ebola ndugu:
Dk Mfaume amesema virusi vya ugonjwa Ebola na Marburg ni familia moja kisanyansi namna njia ya kuambukiza zinafanana, watu waliokuwa hatari zaidi ni watu ambao walikuowa na mgonjwa muda mrefu.
“Ugonjwa huu unaambukiza mtu akiwa na dalili tofauti na Covid 19 mtu anaweza kukuambukiza hata kama hana dalili.
“Virusi vya marburg vinapatikana katika kila aina ya maji maji iwe ni jasho, iwe ni mate, iwe ni matapishi, iwe kufanya mapenzi na mtu ambaye tayari ameathirika.”Amesema
Dalili za Marburg
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili. Unaanza ghafla na homa, kuumwa kichwa, kuumwa misuli, kuumwa tumbo na kichefuchefu