SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), itatumia zaidi ya Sh bilioni Saba katika ujenzi wa daraja jipya la Berega wilayani Kilosa, Morogoro.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofanywa na Bodi ya Ushauri ya TARURA Mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa bodi hiyo Florian Kabaka, amesema ujenzi wa daraja hilo utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Berega na maeneo mengine waliokuwa wakipata tabu baada ya daraja la awali kuvunjika .
“ Daraja hili linagharimu zaidi ya shilingi bilioni saba na ni moja kati ya madaraja makubwa kabisa ambayo TARURA inatekeleza ujenzi wake kwa kutumia fedha za tozo. Sisi kama bodi tunaridhika na namna mradi unavyoendelea, ambapo tunaambiwa umefikia asilimia 72 na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2023, “ amesema
Ameeleza kuwa daraja hilo litaleta ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Berega kwa sababu litawaunganisha na maeneo mengine kama Gairo, Dodoma na Tanga, pamoja na kuwarahisishia wananchi kufika Hospitali ya Wilaya ya Berega.
Naye Kaimu Meneja wa TARURA, Mkoa wa Morogoro Benjamon Maziku amesema kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi Berega na Wilaya ya jirani ya Kilindi kwa sababu litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya aina yote, hivyo kuwarahisishia usafiri na usafirishaji wa mazao.
Kwa upande wake Michael Majoro, mkazi wa Berega amesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo itakuwa ni faraja kubwa sana kwao, kwani itawaondolea matatizo mengi yaliyokuwa yakiwakabili hasa nyakati za mvua.
“Kwakweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa daraja hili, hapa wapo waliokufa, mifugo kusombwa na maji, wamama kujifungulia ng’ambo ya pili kutokana na kushindwa kuvuka wakati hospitali ipo hapo karibu tu. Mheshimiwa hapa ametukomboa kwa kweli tunaona hili ni daraja la kisasa kabisa na lipo juu,” amesema.
Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Berega unahusisha ujenzi wa Daraja lenye urefu wa meta 140, barabara mkaribio za daraja mete 600 na maboresho ya barabara kutoka Berega kwenda Dumbalume kilometa saba(km 7) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.