Darasa la saba 1,384,340 kuanza mitihani kesho 

 

JUMLA ya watahiniwa 1,384,340 wanaanza kufanya mtihani wa darasa la saba Tanzania Bara kwa siku mbili kuanzia kesho.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Athumani Amasi, amesema watahiniwa hao wanafanya mtihani huo katika jumla ya shule 17,943 na kuwa kati ya watahiniwa hao 661,276 ni wavulana na 723,064 ni wasichana.

Amesema asilimia 95.74 ya watahiniwa hao ambayo ni 1,325,433 wanafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na asilimia 4.26 ambayo ni watahiniwa 58,907 wanafanya mtihani huo kwa lugha la Kiingereza.

Advertisement

Watahiniwa wenye mahitaji maalum wapo 4,221 kati yao 101 ni wasioona, 1,198 ni wenye uoni hafifu na 962 ni wenye uziwi, 487 ni wenye ulemavu wa akili na 1,473 ni wenye ulemavu wa viungo mwilini.

Amesema mtihani huo unafanywa katika jumla ya masomo sita ambayo ni Kiswhaili, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Lugha ya Kingereza, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi pamoja na Uraia na Maadili.

“Maandalizi ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, karatasi maalum za kujibia mtihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika halmashauri na manispoaa zote,”amesema Amasi.

Hivyo ametoa onyo kwa walimu wakuu, waratibu elimu kata, wamiliki wa shule,wasimamizi wa wakuu na wa mkondo kutojihusisha na njama za udanganyifu katika mtihani huo na yeyote atakayebainika kufanya hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.