DART yajipanga kwenda nje ya Dar es Salaam

WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umesema mchakato wa kuwa na sheria inayoruhusu kutoa huduma nje ya Mkoa wa Dar es Salaam upo ngazi ya wizara.

Ofisa Habari wa Dart, Elias Malima alisema kwa sasa ni vigumu kwa DART kutoa huduma ya usafiri kwa mikoa mingine kwa kuwa sheria ya sasa inayosimamia huduma hiyo inaruhusu kwa Mkoa wa Dar es Salaam tu.

“Ni kweli tulipata maagizo ya kutanua wigo kwa kupeleka huduma hii mikoa mingine ila ni ngumu kwa kuwa sheria ambayo inasimamia huduma hizi, inaruhusu Mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa na ndio mana unaona hata jina la mtoa huduma ni Usafiri Dar es Salaam Rapid Transport (DART) ila mchakato ushaanza na sasa upo katika ngazi ya wizara ukikamilika utapelekwa Bungeni ukupita basi tutaifikia mikoa mingine,” alisema Malima.

Alilieleza HabariLEO kuwa DART imefanya tathimini kuhusu eneo gani lifuatie kupata huduma ya mabasi yaendayo haraka baada ya sheria kukamilika na utafiti wao umeonesha Majiji ya Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya na Makao makuu ya nchi Dodoma yanahuitaji mkubwa kutokana na idadi ya kubwa ya watu.

Akizungumzia hatua ya pili mradi huo ambao utatoa huduma ya usafiri kati ya Gerezani Kariakoo na Mbagala alisema ujenzi wa miundombinu uko katika hatua za mwisho.

Alisema awali mkandarasi huyo aliomba kuongezewa miezi sita baada ya muda wa awali kuisha lakini serikali ilikataa na kuongezea miezi mitatu ambayo nayo imekwisha.

“Mkandarasi aliomba aongezewe miezi sita lakini serikali ilikataa ikamuongeza mitatu ambayo nayo imekwisha, hivyo tutakaa nae na tuone nini kitaendelea kwa kiwa nia yetu ujenzi huo ukamilike haraka ili wananchi wapate huduma,” alisema Malima.

Alisema kwa sasa wamengia makubaliano na Tantrade kutoa huduma ya usafiri kutoka Mbagala kwenda Gerezani na huduma hiyo itakoma baada ya kumalizika maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Januari 2 mwaka jana wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki aliutaka Wakala wa DART kutumia uzoefu ulioupata Dar es Salaam kuanzisha huduma kama hiyo katika miji mikubwa mingine inayokabiliwa na msongamano wa magari.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button