Dawasa wapewa maagizo matano

NAIBU Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Christina Mndeme ametoa maagizo matano kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) likiwemo agizo la kujenga eneo la kutibu maji machafu kabla hajaenda baharini.
Maagizo mengine ni pamoja na kuhakikisha wanatenganisha mfumo wa maji machafu na maji safi ya mvua na kuziba bomba la maji machafu lililo katika eneo la Ocean Road lililotobolewa na kutiririrsha maji machafu yanayosambaza harufu mbaya.
Alitoa maagizo hayo jana alipotembelea fukwe zilizo karibu na Hospitali ya Aga Khan hadi Ocean Road ambako kumekuwa na harufu mbaya inayosambaa na kuwakera wananchi walio katika maeneo hayo na wapita njia iliyosababishwa na maji machafu.

Alisema ili kulinda mazingira ya bahari ni muhimu maji yanayoenda baharini yawe yametibiwa na kutoa miezi mitatu kwa Dawasa kuanza utaratibu wa kujenga na kukamilisha eneo hilo la kutibu maji ili kuondoa kero iliyopo.
“Ninawaelekeza Dawasa kujenga eneo la kutibu maji machafu ili maji yatakayoenda baharini yawe yametibiwa na tutakuwa tumejikinga na uwezekano wa kupata magonjwa yanayoweza kutokea,” alisema Mndeme.
Aliagiza wahakikishe mfumo wa maji taka ujitegemee bila kuingilia wa maji ya mvua na kuhakikisha maji taka yanatibiwa.
“Tumeona katika eneo la Gymkana kipo kituo cha kusukuma kuyaleta maji machafu kwenye mfumo wa maji machafu lakini kile kituo hakitibu maji, tunahitaji sasa yale maji yatibiwe. Yale maji machafu yanapoingia baharini yawe yametibiwa kwasababu bahari ni uchumi Bahari, bahari ni uhai na utalii,” alifafanua.
Kuhusu bomba lililotobolewa katika eneo la Ocean Road, aliagiza lizibwe kuzuia maji machafu yanayotiririrka na kusambaza harufu.
“Pia hakikisheni makazi yote ya taasisi na watu binafsi mifumo yao yote ya maji machafu inaunganishwa katika mfumo wenu wa maji machafu ili kuondoa mwingiliano kati ya mfumo wa maji taka na maji safi ambao umejengwa na watu wa jiji,” aliagiza.

Vilevile, alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya kupanda miti ambayo ni rafiki katika eneo la fukwe hizo ambayo itaweka mazingira ya fukwe katika hali nzuri na ya kuvutia na rafiki kwa viumbe wa bahari.
Awali, akieleza walichogundua baada ya kutembelea eneo hilo alisema, tatizo kubwa ni mfumo wa maji machafu kutoka katika makazi na taasisi ambayo huingiliana na mfumo wa maji safi ya mvua na kuwa mifumo hiyo imeingiliana na kusababisha maji machafu kutoenda yanakostahili na kushia njiani.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya alisema watashirikiana na Dawasa kubaini wanaounganisha mifumo ya maji taka kwenye mifumo wanayoisimamia yam aji ya mvua na kuimarisha mifumo ya kuleta maji baharini ili ifanye kazi inavyotakiwa.



