Dk Gwajima kuongoza maadhimisho Siku ya Wanawake Geita

GEITA: WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Dorothy Gwajima anatarajia kuongoza maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani yatakayofanyika mkoani Geita.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuambatana na uzinduzi wa mradi wa PAMOJA unaolenga kukuza usawa na kutokomeza ukatili wa kijinsia kupitia uwezeshaji wanawake kiuchumi na kijamii.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela ametoa taarifa hiyo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geita na kueleza Geita imechaguliwa na Wizara kuwa mwenyeji wa kilele cha maadhimisho hayo Machi 08, 2026
Amesema maadhimisho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, “Haki Sawa kwa wanawake na Wasichana, Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya 2050”.
Amesema kauli mbiu hiyo inalenga kuikumbusha jamii juu ya wajibu wa pamoja kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki, fursa na ulinzi stahiki ili kufikia maendeleo endelevu.
Shigella ameeleza ili kufanikisha hilo mkoa umejizatiti kutumia maadhimisho hayo kuimarisha huduma kwa wahanga wa ukatili, pamoja na kuboresha malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto.
“Kuanzia Machi 06 mwaka huu huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za kibenki, msaada wa kisheria, Bima ya Afya, Huduma za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
“Pia kutakuwa na Dawati la Jinsi ana Watoto pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, hii ni fursa adhimu kwa wananchi kupata huduma kwa ukaribu na urahisi zaidi sehemu moja”, amesema.
Amesema mkoa pia utatumia maadhimisho hayo kama jukwaa la kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini na miradi ya kitaifa kupitia uwezeshaji utakaofanywa na wakufunzi tofauti.



