DC Arusha amaliza mgogoro kiwanda cha Lodhia

DC Arusha amaliza mgogoro kiwanda cha Lodhia

MKUU wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amemaliza mgogoro wa wafanyakazi zaidi ya 500 wa kiwanda cha kutengeneza chuma cha Lodhia Group kilichopo jijini Arusha.

DC Mtahengerwa amesema kulikuwa na malalamiko ya kutishiwa bastola, kufanya kazi ngumu na kulipwa mshahara mdogo, hivyo amekutana na menejimenti ya kiwanda na kukubaliana mambo mbalimbali yanayohusu haki za wafanyakazi, ikiwemo vikao vya wafanyakazi.

Amewataka wafanyakazi hao kuendelea na kazi kwani serikali imekubaliana na menejimenti hiyo katika kuhakikisha maslahi bora ya wafanyakazi, yanaboreshwa ikiwemo mishahara na malipo ya ziada ya kazi.

Advertisement

“Kuna mambo ya kiutumishi tumewekana sawa ikiwemo uwepo wa vifaa vya kazi zinavyokidhi ubora wa kazi na waliotoa hoja za madai mbalimbali, wasifukuzwe bali wafanye kazi na kama wakifukuzwa wawe wamefanya makosa mengine na si haya ya haki zao,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni za Lodhia Group, Harun Lodhia amesisitiza yaliyotokea yamesawazishwa na lengo kubwa wafanyakazi wapate ajira na kuahidi kuongeza fedha kwa wafanyakazi, ikiwemo kiwango cha mshahara kwa kada zote za wafanyakazi wa kiwanda cha kutoka Sh150,000 hadi Sh 180,000 na kusisitiza wafanyakazi kufanya kazi pale wanapolipwa mishahara yao.

“Kila mwaka mara mbili watafanya vikao na wafanyakazi hao, naomba tusameheane sisi sote ni binadamu tufanye kazi na mkipata mshahara msilale njooni kazini,” amesema.