DC Bukoba aonya viongozi uharibifu vyanzo vya maji

MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Siima, amesema hatawafumbia macho viongozi wa vijiji na mitaa na kata watakaoshindwa kusimamia sheria za vyanzo vya maji na kuruhusu wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji.

Alisema hayo wakati akikagua mradi wa maji wa Kibirizi, ambao umevamiwa na wananchi wanaendelea kulima ,kuuziana  eneo la mradi wa maji na kuharibu miundombinu ya maji, ambapo shughuli hizo zinasababisha upungufu wa maji katika mradi huo.

Mkuu wa wilaya ambaye aliongozana na kamati ya ulinzi na usalama, aliagiza kushikiliwa kwa wananchi wawili wa Kibirizi  kwa ajili ya mahojiano, baada ya familia moja ambayo ilitoa eneo  kujenga mradi wa maji mita 70   mwaka 2016 na hivi karibuni kuonekana linadai eneo hilo kwa nguvu na kuanza kulima na kumega vipande na kuviuza.

“Nimefika na Kamati ya Ulinzi na Usalama , tumekagua mamilioni ya fedha za serikali yaliyotolewa kwa ajili ya kuleta mradi wa maji, lakini amekuja mtu amelima mpaka ndani  ya mradi huu na amepanda mazao.

“Maji yanapungua katika vyanzo vyetu kwa ajili ya watu wachache , niseme imenisikitisha sana, hatuwezi kuvumilia lazima waliofanya hivi wakatueleze pale polisi kwamba wanafanya hivi kwa lengo gani? Amehoji Siima.

“Nina barua zote ambazo mwenye hilo eneo alitoa kwa sababu kijiji hiki kilikuwa na uhitaji wa maji, Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la msingi mwaka 2016,  Aweso (Juma) Waziri wa Maji alitembelea  mradi.

“Aliyetoa eneo amefariki mwaka jana, halafu imetokea familia imelima mpaka ndani ya chanzo cha maji, na kuuza eneo hili kwa madai kuwa aliyetoa eneo tena alikuwa Diwani wa kata hii ya Kibirizi kuwa hayakuwa makubaliano, siwezi kukubali nitawashikilia mpaka watoe maelezo vizuri aliyelima na aliyenunua eneo la mradi tunaondoka nao leo, “alisema.

Mkuu wa Wilaya alikemea tabia za baadhi ya wananchi wanaotumia nafasi vibaya kuchukua maeneo katika taasisi za umma kuendesha shughuli zao, ambapo ameahidi kuanzia sasa hawezi kuvumilia.

 

Kupitia ziara hiyo amezindua mradi wa maji wa Omukihisi Kata Kyamulaile,  wenye thamani ya Sh Milioni 280 utakaowahudumia wananchi 2460, ambapo aliwataka wananchi kutunza na kusimamia mradi huo na kujiepusha na uharibifu wa miundombinu.

Alitoa wito kwa kamati ya maji kuhakikisha fedha zinazotokana na uchangiaji wa maji ya mradi huo zinatumika kuendesha mradi huo na sio vinginevyo.

Meneja wa Wakala wa maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Halmashauri ya Bukoba,  Erasto Mgaya alisema kuwa upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Bukoba  ni asilimia 74, ambapo miradi mikubwa ya maji inaendelea kutekelezwa, ili kufikia asilimia 85 ya upatikanaji maji safi na salama ifikapo mwaka 2025.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button