DC Geita atoa angalizo matumizi ya fedha za maji

MKUU wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo ametoa angalizo kwa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) kuzingatia uadilifu wa matumizi sahihi ya mapato ya miradi ya maji ili kuendeshwa kwa tija.

Shimo ametoa angalizo hilo leo wakati akifungua Mkutano mkuu wa Kwanza wa Mwaka kwa viongozi wa CBWSOs wilayani Geita chini ya uratibu wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Amesema serikali inatarajia kuona CBWSOs wanakuwa muhimili wa kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika huduma, kuendeleza miradi ya maji vijijini pamoja na kuondoa migogoro ya huduma ya maji ndani ya jamii.

“Onyesha mabadiliko, onyesha nia, ya kwamba hata baada ya kukabidhiwa mradi huu wewe na kamati yako ndani ya bodi yako, na nyinyi sasa kupitia makusanyo yenu, muongeze mtandao mwingine, kwa watu wengine.

“Haipendezi kwamba sisi ambao ni viongozi na wajumbe wa bodi ya kamati ya maji tukaonekana tumekuwa tena shida ya fedha ambazo zinakusanywa na zinapatikana baada ya kuuza maji katika miradi yetu.”

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Geita, Mhandisi Sande Batakanwa amesema wamejipanga kusimamia matumizi ya ‘Control namba’ kukusanya mapato ya maji kutoka CBWSOs ili yaweze kutumiwa kwa usahihi.

Amesema mbali na pesa za CBWSOs wanaendelea kusimamia vizuri vizuri ya pesa za serikali kutatua kero ya maji ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita walipokea jumla ya Sh bilioni 2.2 na kuimarisha huduma ya maji hadi asilimia 57.

“Lakini tuna miradi takribani sita ambayo inaendelea, mingine ipo hatua ya asilimia 98 na mingine 99 na wananchi wanapata huduma. Tunatarajia miradi yote hii ikianza kutumika tuna mategemeo ya kufikia asilimia 62 mpaka 65.

Mwenyekiti wa CBWSOs kata ya Nyakagwe, Elizabeth Maige ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu kwa kuimarisha huduma ya maji na kumuhakikishia usimamizi thabiti wa miradi ya maji ili kufikia malengo ya serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button