DC Mwenda amzawadia pikipiki mwalimu

MKUU wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Yusuph Mwenda amemkabidhi pikipiki Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Milambo iliyopo kijiji cha Mingela Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui wilayani Iramba, Mwalimu Hussein Kionda, kwa lengo la kuondoa changamoto ya usafiri unaomkabili mwalimu huyo.

Mwenda ameyasema hayo Novemba 1,2024 wakati akimkabidhi pikipiki huyo nje ya viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kuhudhuriwa na Kaimu Ofisa Elimu idara ya Elimu Awali na Msingi Agnes Peter.

Advertisement

DC Mwenda amesema kutokana na changamoto ambayo ilikuwa inamkabili mtumishi huyo kutoka na ukosefu wa miundombinu ya barabara na hakuna usafiri wa aina yoyote unaoweza kufika eneo hilo na hakuma huduma muhimu, ilimfanya mtumishi huyo kupata shida ya kufika na kufanya kazi zake ipasavyo.

“Malengo ya Wilaya ya Iramba katika ufaulu ni kufika asilimia 100 % na kwa sasa tupo kwenye asilimia 77% hivyo tukio hili litakuwa endelevu kwa shule zote na kuhakikisha kuwa tumeziondoa. Tumekuwa tukitoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri kitaaluma mwaka huu tulitoa kompyuta kwa kila shule zilizofanya vizuri kitaaluma kwa kata 20,”amesema DC Mwenda.

DC Mwenda amempongeza Ofisa Elimu idara ya Elimu Awali na Msingi Mwalimu, Rose Kibakaya, kwa kuwa msikivu katika kupanga mikakati ya kuinua ufaulu kwa kuhakikisha tunatoka motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri.