DC Nzega asisitiza wanafunzi kwenda shule bila sare

MKUU wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai ametoa wito kwa wananchi wote kuwapeleka shule watoto wasio na sare za shule, daftari na vifaa vingine vya shule au kufika ofisini kwake kwa msaada.

“Ukiona mtoto sehemu haendi shule kisa sare za shule, daftari na vifaa vingine vya shule, muelekeze aje Ofisini kwangu nitamuhudumia kwa mahitaji ya shule,” alisema Tukai.

Ofisa Tarafa wa Nyasa, Ricardo Komanya amepongeza juhudi za Tukai na kuwataka viongozi wote wa Tarafa ya Nyasa kuhakikisha wanawapa maelekezo sahihi wahitaji wote wa tarafa hiyo.

“Nachukua fursa hii kuunga mkono juhudi za Mkuu wa Wilaya yetu kwa kutoa maelekezo kwa viongozi wa Kitongoji, Kijiji, Mtaa, na Kata kuhakikisha wanawahamasisha wananchi wenye mahitaji kufika ofisini kwa Mheshimiwa Tukai,” alisema Komanya.

Pia, Viongozi wa ngazi mbalimbali wameombwa kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa wahitaji wote ili kupunguza tatizo la ukosefu wa vifaa vya shule kwa watoto wa tarafa ya Nyasa na Wilaya ya Nzega kwa ujumla.

“Muhimu sana; Kwa wananchi wenzangu wa Tarafa ya Nyasa, nitafatilia utekelezaji wa fursa hii na kupokea malalamiko moja kwa moja kutoka kwenu,” aliongeza Komanya.

Utekelezaji wa wito huu unalenga kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya msingi ya elimu bila vikwazo vya vifaa vya shule.

Habari Zifananazo

Back to top button