Ataka uadilifu ujenzi wa Sekondari Kagunga

Wananchi wa Kijiji cha Kagunga Kata ya Kasekese Halmashauri ya Wilaya Tanganyika mkoani Katavi, wameishukuru serikali kwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule ya Sekondari Kagunga.

Wametoa shukrani hizo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu aliyeoongozana na viongozi mbalimbali katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la mradi wa shule hiyo alipofika kuzindua shughuli za ujenzi.

Akiwahutubia wananchi, Buswelu amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia mradi huo, mafundi pamoja na wataalamu kusimamia kwa weledi kwani kuanzia sasa anataka kuiona Tanganyika mpya yenye usimamizi mzuri wa miradi yenye ubora kuliko wakati mwingine.

Amewataka wananchi, mafundi pamoja na wazabuni waliopewa tenda za kusambaza vifaa vya viwandani yakiwemo matofali, mawe, mchanga na kokoto kuwa wazalendo kwa kuhakikisha mahitaji yote yanafika kwa wakati na amekemea wizi wa rasilimali za mradi huo, kwani atakayebainika kuhujumu mradi huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

DC Buswelu amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Shaban Juma kuhakikisha anatimiza wajibu kwa kufanya malipo kwa wakati pasipo usumbufu kwa kila hatua ambayo malipo yanatakiwa kufanyika kwa mujibu wa mkataba.

“Sio fundi akishaanza kupiga plasta, anaweka marumaru halafu bado anadai hela ya msingi, hiyo biashara ife kabisa, fedha zipo zimetolewa za kutosha na zitumike ili kukamilisha mradi kwa wakati,” amesisitiza Buswelu

Pia ameagiza baadhi ya vifaa vianze kufikishwa eneo la mradi, lengo likiwa ifikapo Oktoba 15, 2023 ujenzi uwe umekamika ukiwa na vyumba vya madarasa vinne na ofisi , ambavyo kati yake kutakuwa na ofisi za walimu mbili, jengo la utawala na majengo matatu ya maabara ya masomo ya biolojia, kemia na fizikia, maktaba, jengo la tehama na vyoo matundu 4 kwa ajili ya wavulana.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Dk. Alex Mrema amesema tayari ujenzi wa mradi huo umeanza na wanategemea utakamilika kwa wakati.

Dotto Mwelela mkazi wa Kijiji hicho cha Kagunga amesema kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia watoto wao kutotembea umbali wa takribani kilometa 10 kufuata masomo katika shule ya Sekondari Kasekese.

Habari Zifananazo

Back to top button