Dereva, kondakta washikiliwa usafirishaji vipodozi hatari

POLISI mkoani Mbeya imemkamata dereva na kondakta wake wakisafirisha shehena na vipodozi vyenye viambata vya sumu kwa kutumia lori la mafuta.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema watuhumiwa hao ambao ni wakazi wa Dar es Salaam, walikamatwa wakiwa na gari yenye namba za usajili T 900 DEV aina ya Axon Benzi mali ya Kampuni ya Feet Logistic Ltd ikiwa na tela lenye namba T 800 DEL.

Alimtaja dereva wa lori hilo la mafuta ni Fahmi Ahmed (33) ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Kigamboni Soweto na kondakta wake, Mohamed Mawazo (26), mkazi wa Mabibo, mkoani Dar es Salaam.

Kamanda Kuzaga alisema walikamatwa wakiwa wamepakia makasha 1,052 ya vipodozi vya aina mbalimbali vyenye viambata vya sumu na vilivyopigwa marufuku kuingizwa nchini.

Alisema watuhumiwa walikamatwa Machi 25 mwaka huu saa 3:00 asubuhi eneo la Kijiji cha Songwe, Kata ya Bonde la Songwe, Tarafa ya Usongwe, wilayani Mbeya.

Walikamatwa baada ya polisi kupata taarifa za siri na kuweka mtego uliofanikisha kuwatia mbaroni wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuingiza nchini.

Alitaja vipodozi walivyokamatwa navyo na idadi ya makasha kwenye mabano ni epiderm (38), coco pulp (159), citro light (87), caro light (152), prety white (22), coco pulp maji (100), gluta white (59), diproson (41), pawpaw (91), extra clair (50), clear therapy Ct + (164), betason (72) na nacitro light (87).

Alisema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa huku gari waliyokamatwa nayo ikishikiliwa na polisi na baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani.

 

Habari Zifananazo

Back to top button