TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeanza kutekeleza mradi wa kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao wenye thamani ya Sh milioni 131.
Mratibu wa mradi huo, Dk Stephen Wambura alisema umepatikana baada ya taasisi hiyo kushinda kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania kupitia Mfuko wa kuendeleza Ujuzi (TEA-SDF).
Alisema lengo ni kutoa mafunzo kwa wahitimu wa vyuo wasiokuwa na ajira waliopo mtaani waweze kujiajiri na kuajiri wenzao.
Alisema katika awamu ya kwanza, taasisi hiyo inatoa mafunzo ya ufundi simu kwa njia ya mtandao, lengo likiwa ni kupata wanafunzi 300 kwa mradi mzima. Alisema waombaji walifika zaidi ya 3,000.
“Kwa sababu maombi yalikuwa mengi waliopata nafasi na kukidhi vigezo ambao mpaka sasa wanaendelea na mafunzo ni wanafunzi 592,” alisema. Mafunzo hayo ni ya mwezi mmoja na mhitimu atapatiwa cheti.