Dk Biteko aagiza walimu kupewa motisha

DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameziagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMi kuangalia utaratibu mzuri wa kuwapa motisha Walimu na hii ikihusisha kutenga walau siku moja ya kuwapa Motisha walimu hao badala kusubiri Mei Mosi kwa lengo la  kupata matokeo yaliyo bora kwenye Sekta ya Elimu.

Akiwa katika hafla ya kuzindua Programu ya Kuboresha Kada ya Ualimu nchini (GPETSP) katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Dk Biteko amempongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (GPE), Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete na kueleza kuwa nafasi aliyonayo ni heshima kwa nchi pamoja na Sekta ya Elimu nchini kwani amekuwa na mchango katika kuhakikisha nchi inafaidika na mfumo wa GPE ambao unahudumia nchi 89 duniani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya GPE, Dk Kikwete amesema kuwa, lengo la Taasisi hiyo ni kusaidia kuchochea maendeleo ya elimu  katika nchi zinazoendelea hasa za kipato cha chini na za kipato cha kati hatua ya kwanza ambapo Tanzania ni moja ya nchi 89 wanufaika wa GPE.

Advertisement

Amesema kuwa, kutoka GPE ianze mwaka 2002 imeshachangia Dola milioni 330  nchini Tanzania na kwamba GPE inaunga mkono juhudi za Serikali kuboresha Sekta ya Elimu ili kila mtoto nchini awe na ujuzi na maarifa na sasa Taasisi hiyo imeidhinisha ufadhili wa Dola za Marekani Milioni 80 kwa ajili ya programu ya GPETSP.

Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema kuwa, programu iliyozinduliwa ya GPETSP inagusa sehemu mbalimbali katika Kada ya Ualimu ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na utoshelevu wa  Walimu, ubora, uwepo wa miundombinu, vitendea kazi, kuendeleza makazi ya walimu  na motisha kwa walimu na kwamba Serikali imekuwa ikiyafanyia masuala hayo lakini GPETSP inakuja kuongeza nguvu na  kasi ya utekelezaji wa programu za Serikali ikiwemo Sera ya Elimu.