Dk Biteko atoa maagizo kumaliza kuadimika kwa Dola

DAR ES SALAAM: KUADIMIKA kwa dola ya Kimarekani nchini, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameagiza kuongezwa kwa mauzo ya samaki nje ya nchi ili ziwapate fedha za kigeni ambazo zimekuwa changamoto kubwa kwenye uchumi wa nchi.

Pia, amewaagiza watendaji wa Sekta ya Uvuvi nchini kuifanya Sekta hiyo kuwa nyenzo muhimu ya kuondoa umaskini nchini.

Amesema, lengo ni kuiwezesha Sekta ya Uvuvi iwe na mchango mkubwa kwa wananchi na Taifa wa ujumla.

Dk. Biteko ameyasema hayo  Oktoba 26, 2023 wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) sambamba na kuzindua mfumo maalum wa upatikanaji wa taarifa sahihi za uvuvi na kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya TAFIRI na ZAFIRI kwenye mazao ya bahari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema, kuna haja ya kuongeza mchango wa mauzo kwa bidhaa nje ya nchi ili kuweza kuleta fedha zaidi za kigeni ambayo imekuwa changamoto kubwa kwenye uchumi wa nchi.

Amesema kuwa, “Mauzo ya bidhaa yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 168 mwaka uliopita hadi kufikia Dola za Marekani milioni 249,” ameeleza Dk. Biteko.

Dk Biteko amesema hata hivyo mchango mkubwa katika sekta hiyo ya Bahari ni mauzo kutoka maji baridi kwa asilimia 85 na kwamba mchango wa Bahari bado ni mdogo na kuitaka TAFIRI kufanya kazi ya ziada kuisaidia wizara na taasisi za serikali kuhakikisha uvuvi kwenye bahari kuu unaongeza mchango wake ili kuongeza mauzo.

“Nchi yetu imejaliwa maziwa makubwa, bahari na mito kuliko nchi nyingine zinazotuzunguka tunatumiaje hizi fursa kuondoa umaskini wetu na kuwavutia watanzania kukimbilia sekta ya uvuvi na kuondoa umaskini?”amesema kwa kuhoji na kuongeza
“Waziri Ulega bado una kazi kubwa ya kufanya, unatakiwa kuyatafsiri mambo hayo kwa vitendo ili wavuvi wanafaike kupitia sekta hiyo.” Amesema Biteko.

Habari Zifananazo

Back to top button