WAZIRI wa Maliasili na Utali, Balozi Dk Pindi Chana amemwagiza Kamishina wa Wakala wa Huduma na Misitu (TFS) Professa Do Santos Silayo kuhakikisha idara hiyo inakujikita katika kukusanya mapato kupitia mfumo Tehama ili idara hiyo iongeze mapato.
Balozi Dk Chana ametoa agizo leo Novemba 5, alipofungua Mkutano Mkuu wa Tatu wa Makamanda wa TFS jijini Arusha. Amesema malengo waliyovuka ya kukusanya mapato ya Sh bilioni 166 sawa na asilimia 103 kama wangekuwa wanatumia mfumo wa Tehama malengo hayo yangekuwa makubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.
Amesema pamoja na kuipongeza TFS kwa kuvuka malengo ya makusanyo ila ameitaka taasisi hiyo kukusanya mapato kwa mfumo wa Tehama kwani idara nyingi za serikali zimejikita katika mfumo huo.
Waziri Chana amesema hadi Juni mwaka huu, TFS ilikusanya zaidi ya Sh bilioni 166 na kuvuka malengo yaliyokusudiwa: “Hivyo pongezi za dhati kwa menejimenti chini ya Kamishina Silayo na bodi lakini jitihada za ziada zinahitahija katika ukusanyaji mapato.
”Ninakuomba Kamishina sasa mnapaswa kubadilika na kukusanya mapato kwa mfumo wa Tehama ili mapato yawe mengi na salama na malengo yaliyokusudiwa yazidi kupaa kwa asilimia zaidi ya mia moja,” amesema Balozi Chana.
Akizungumzia uadilifu katika kazi, Balozi Dk Chana aliwataka makamanda wa TFS kufanya kazi kama makanda wa jeshi kama walivyo baada ya kutoa katika mfumo wa uendeshaji kiraia ikiwa ni pamoja na kuwa wazalendo katika kazi na kufuata kanuni na sheria za taasisi.
Balozi Dk Chana amesema sifa kuu ya askari kwanza ni kuwa mzalendo, muadilifu na muaminifu hivyo makamanda wa TFS wanapaswa kwenda sambamba na misingi hiyo ili kulinda misngi ya kazi katika uendeshaji kazi za kila siku ili serikali iendelee kuwaamini.
Amesema TFS inapaswa kufanya kazi kisasa ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kununuwa vitendea kazi vya kisasa ikiwa ni pamoja na magari ya kisasa, ndege na helkopta vyote vinahitajika katika utendaji kati katika misitu.
Waziri huyo amesema kuwa pamoja na hayo ameitaka menejimenti na Bodi ya TFS kuhakikisha wanatatua changamoto za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawapandisha vyeo wanapostahili na kuongezewa maslahi kwa wakati.
Amesema watumishi wa TFS wakiangalia kwa jicho la tatu katika maslahi shughuli za utendaji kazi za kila siku za Taasisi hiyo zitazidi kusonga mbele na makusanyo ya mapato ya serikali yatakuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kwa kuwa wafanyakazi wanatatuliwa changamoto zao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TFS, Brigedia Jeneral Mbaraka Naziad Mkeremy amesema kuwa TFS imejipanga kuhakikisha malengo ya makusanyo ya kila mwaka yanafikiwa na kuzidi ili taasisi hiyo iweze kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kuhakikisha taasisi hiyo inatatua changamoto za jamii.
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi, Mhandisi Enock Nyanda ambaye ni mjumbe wa Bodi ya TFS alisema kuwa Bodi kwa kushirikiana na menejimenti imekuwa ikishirikiana katika kuhakikisha inajali maslahi ya wafanyakazi na kutatua changamoto zinazowakabili.
Mwenyekiti wa Bodi amesema kuwa TFS imekuwa ikishirikiana na jamii katika kutatua changamoto lengo ni kutaka jamii kuishi kwa kufata kanuni na sheria za misitu na nyuki.