Dk Kijaji awasili Zimbabwe kushiriki mkutano wa utalii

ZIMBABWE: Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji leo Aprili 28, 2026 amewasili nchini Zimbabwe kushiriki Mkutano wa Pili wa Kikanda wa Shirika la Utalii Duniani.

Mkutano huo unalenga kuimarisha uwezeshaji wa wanawake katika sekta ya utalii barani Afrika na unatarajiwa kufanyika katika eneo la Victoria Falls kuanzia Aprili 29 hadi Mei 1, 2026.

Mara baada ya kuwasili, Dk Kijaji amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Balozi Suzan Kaganda.

Mkutano huo unalenga kujadili fursa zilizopo, changamoto zinazowakabili wanawake, pamoja na mikakati ya kuongeza ushiriki wao katika sekta ya utalii na kuchangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa nchi za Afrika.

Katika mkutano huo, Dk Kijaji anatarajiwa kuwa mzungumzaji katika mdahalo wa mawaziri, ambapo viongozi wa ngazi za juu watajadili namna ya kuimarisha nafasi za wanawake katika uongozi na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika sekta hiyo.

Sambamba na hayo, mkutano huo utahudhuriwa na wadau mbalimbali wa utalii kutoka ndani na nje ya Afrika, ukiwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujadili sera bora, na kuweka mikakati ya kukuza utalii jumuishi na endelevu. Ajenda kuu zitajumuisha kuimarisha uongozi wa wanawake, kukuza ujasiriamali na kupanua fursa za kiuchumi ili kuongeza mchango wao katika ukuaji wa sekta ya utalii barani Afrika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button