DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Vunjo Dk.Charles Kimei ameishauri serikali kubadilisha mfumo wa utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi na badala yake mikopo hiyo itolewe kwa mtanzania mmoja ambaye anawazo zuri la kufanya shughuli yoyote itakayomuwezesha kufanya marejesho kwa wakati na kuingizia serikali mapato yatakayoweza kuzungusha fedha hizo kwa wengine.
Akichangia Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa Kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma Katika Serikali za Mitaa LAAC iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma,Dk. Kimei amesema mfumo wa utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi bado utaendelea kuwa shida hasa katika urejeshaji wa mikopo hiyo na utaendelea kuingizia serikali hasara .
“ Ukimpa mtu mmoja ambaye ana wazo lake zuri na ukamuuliza maswali machache ya shughuli yake pia anaweka akiba kwenye mabenki basi unaweza kumpa mkopo lakini kikundi ni ngumu kidogo halafu huwezi kukifunga kikundi” alisema Dk. Kimei.
SOMA: Msalala waanza kutoa mikopo vijana, wanawake
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ,serikali imeshindwa kukusanya shilingi bilioni 76 kama marejesho ya mikopo ya asilimia kumi iliyotolewa kwa vikundi katika Ofisi mbalimbali za Halmashauri.