Dk.Kiruswa awapa neno wadau sekta ya Madini

DAR ES SALAAM, NAIBU Waziri wa Madini Dk. Steven Kiruswa ameutaka ujumbe wa wadau wa Sekta ya Madini wapatao 100 wakiwemo wachimbaji wadogo, wachimbaji wa Kati, Wafanyabiashara wa madini na watoa huduma migodini kuhakikisha inaleta matunda kwa kuleta wawekezaji wengi na kupata vifaa vya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa madini nchini.

Amesema hayo katika hafla fupi ya kuiaga timu hiyo Agosti 11, 2023 jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa, ubalozi wa China kwa kushirikiana na Kampuni ya Touchbroad ya nchi hiyo imeandaa ziara ya wachimbaji kutoka Tanzania ili kuwawezesha kukutana na wawekezaji wa Sekta ya Madini nchini China, kutembelea viwanda vya kutengeneza mitambo na vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini na kuwawezesha kupata uzoefu na wafanyabishara wa madini waliopo China na kupata teknolojia za uchimbaji na uchenjuaji.

“Niwaombe kila mmoja wenu akiwa China ahakikishe anatimiza malengo yake kadri anavyoweza ili ujuzi mtakaoupata uje kuwasaidia kuboresha biashara zenu na kuongeza tija,” amesema Dk. Kiruswa.

Vile vile, amezipongeza taasisi za fedha kwa kuendelea kuwasaidia wachimbaji na wafanyabiashara katika kuhakikisha wanapata mikopo ya fedha kwa kuwa karibu na wafanyabiashara wa madini na amewataka kuangalia uwezekano wa kupunguza riba ili kupata wateja wengi na kuruhusu wachimbaji wadogo kupata mikopo yenye riba ndogo.

Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini nchini (FEMATA), John Bina amesema kuwa, ziara hiyo nchini China inakwenda kufungua milango ya nchi kuvutia wawekezaji wengi kuendelea kuja kwa kuwa nchi ina sera nzuri katika uwekezaji.

 

Habari Zifananazo

Back to top button