Dk Mapana: Hatumvizii msanii tumfungie

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Dk Kedmon Mapana amesema hawamvizii msanii akosee ili wamfungie kwa kuwa suala hilo sio ajenda yao.

Dk Mapana ameyasema hayo Dar es Salaam leo kwenye semina ya wasanii na waandishi wa habari wakifundisha maadili na weledi katika kazi ya sanaa iliyoandaliwa na Basata, Bodi ya Filamu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Kama Basata hakuna kumvizia msanii kwamba akosee ili tumfungie, suala la kufungia sio ajenda yetu lakini tuna wajibu wa kuwapa mafunzo, maelekezo na muongozo na ndio maana tuko hapa,”amesema.

Amesema ni muhimu kukumbushana mambo ya maudhui ili wanapokwenda kuzalisha kazi zao zisiwe na ukakasi bali yajali utu na yawe na uzalendo wa kitaifa.

“Na ndio maana tunawafundisha ni namna gani wasanii wetu wanakuwa wazalendo katika kuitetea nchi yao, hakuna anayeweza kuifanya Tanzania kuwa ya mfano ni Mtanzania mwenyewe,”amesema.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Emmanuel Ishengoma amesema waandishi wa habari wakielewa maadili na miongozo juu ya kazi wanazotengeneza kama hazina maadili hazitaweza kufikia jamii wanayojaribu kuikinga.

Amesema ni muhimu kuelewa ili kupunguza kusambaa kwa kazi ambazo hazitawatambulisha kama Watanzania wastaarabu.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka Bodi ya Filamu Emmanuel Ndumukwa amesema wanatoa elimu ya maadili lengo kuu ni kuwajenga wasanii na waandishi wa habari katika kufanya majukumu yao ili wanapopeleka chakula kwa walaji waweze kupata kitu ambacho ni bora kwa ustawi na kuongezea kipato kwa nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button