Dk Mollel: Tumuunge mkono Rais kwa kuchapa kazi

NAIBU Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, amesema Rais Samia Suluhu  Hassan amefanya mabadiliko makubwa katika kuboresha huduma za afya nchini na kuwataka wauguzi, wakunga na watoa huduma za afya nchini kuunga mkono juhudi  hizo na kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.

“Pochi ya mama ina hela, mama anajua hesabu fedha za corona zilienda kwenye maji ukiweka dola moja kwenye maji unapunguza dola nne kwenye afya na magoli yamefungwa kabla mechi haijaanza, mabadiliko makubwa yanaonekana kila mahali,”  alisema.

Alisema hayo leo wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya  Baraza la Wakunga na Wauguzi Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini hapa.

Alisema kuwa serikali ya Awamu ya Sita imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya nchini, ambapo katika hospitali za kanda kapeleka Sh bilioni 51.8, na kuna maambo makubwa yamefanyika hata kwenye hospitali za mikoa ambazo zimepatiwa  Sh bilioni 54.2.

Wauguzi na Wakunga wakiwa kwenye maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Wauguzi na Wakunga jijiini Dodoma leo. (Picha zote na Sifa Lubasi).

“Katika kununua vifaa imetengwa Sh bilioni 70, lakini tunategemea kupeleka vifaa tiba vya Sh bilioni  100,” alisema

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Profesa Lilian Mselle, alisema kuwa asilimia 75 ya wahitimu wa kada ya uuguzi  na ukunga hawana ajira na kuiomba serikali kuangalia suala hilo kwani ni hasara kwa taaluma.

“Jana (juzi) tulikuwa na mahafali jumla ya wahitimu wa uuguzi na ukunga 1945 walihitimu na kupatiwa vyeti vya usajili na leseni, lakini asilimia 75 kati yao hawana ajira hiyo ni hasara kubwa kwa taaluma,” alisema

Alisema kuwa changamoto nyigine ni kukosekana kwa ajira kwa wahitimu wenye sahada, kwani mfumo wa ajira unawatambua wenye vyeti na diploma.

Mwakilishi wa mganga mkuu wa serikali , Mkurugenzi wa Tiba na Kinga Profesa, Paschal Rugajo alisema kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu na vifaa tiba.

Muuguzi mkuu wa serikali, Ziada Sella alisema kuwa baraza linafanya kazi chini ya sheria iliyoundwa mwaka 2010 na mpaka sasa kuna jumla ya wauguzi 55,000 na waliosajiliwa na baraza ni 42,000.

Habari Zifananazo

Back to top button