MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya YARA wakiongozwa na Rais ambaye pia Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Svein Tore Holsether, mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) Davos Uswisi.
Dk Mpango ameihakikishia kampuni hiyo kwamba serikali itaendelea kuiunga mkono katika shughuli zake nchini Tanzania.
Amesema dhamira ya serikali ni kuendelea kujidhatiti katika kuwa ghala la chakula kikanda kwa kuzingatia ongezeko la watu pamoja na mahitaji ya chakula.
Makamu wa Rais ametoa wito wa kuongeza ushirikiano zaidi baina ya kampuni hiyo na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika miundombinu ya kilimo kama vile maghala, usafirishaji pamoja na umwagiliaji.
Pia amesema ushirikiano unahitajika katika kuimarisha kilimo endelevu ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa na udhibiti wa maji.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema YARA inaweza kushirikiana na Tanzania katika kuwajengea uwezo wakulima wadogo ili waweze kufanya kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji.
Pia amewakaribisha kushirikiana katika tafiti za kilimo, kufanikisha masoko ya mazao ya wakulima na kuongeza ushirikiano na wakulima na vyama vya ushirika na taasisi zingine ili kufanikisha jitihada zilizopo.
Kwa upande wa Kampuni YARA imesema inaunga mkono ajenda ya Afrika ya 2030 ambapo tayari imeweka mkakati wa kushirikiana na mataifa mbalimbali yenye mpango wa muda mrefu katika kuimarisha usalama wa chakula ikiwemo Tanzania.
Kampuni hiyo imedhamiria kuongeza uwekezaji nchini Tanzania na kuongeza ushirikiano katika kuwajengea uwezo wakulima. Tayari kampuni hiyo inashirikiana na mpango wa kukuza kilimo nyanda za juu kusini (SAGCOT) katika kupima afya ya udongo nchini Tanzania.