MAKAMU wa Rais, Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuficha watoto wenye ulemavu majumbani na kuwakosesha haki ya kupata elimu.
Akizungumza wakati akifungua shule ya msingi ya elimu mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar amesema ni vema watoto hao wakapata elimu ili waweze kutumia vipaji walivyonavyo.
Akifafanua alisema serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia ikiwemo ya shule jumuishi.
Aidha, Dk Mpango alisisitia juu ya umuhimu wa rasilimaliwatu akisema ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi ndani ya nchini.
“Sekta ya elimu ni kipaumbele cha serikali zote mbili ili kujenga jamii iliyoelimika na yenye maarifa muhimu,” alisema Makamu wa Rais.