Dk Mpango ampongeza Kardinali Mteule Rugambwa

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amempongeza Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Protase Rugambwa kwa kuteuliwa kuwa Kardinali. Kupitia akaunti ya ofisi ya Makamu wa Rais katika ukurasa wa kijamii wa twitter, Dk Mpango ameeleza kuwa uteuzi huo unathibitishwa na maneno katika Biblia.

“Nimepokea kwa furaha kubwa kuteuliwa kwako na Baba Mtakatifu Fransisco, kuwa Kardinali wa Tatu katika nchi yetu ya Tanzania,” aliandika.

Aliongeza: “Uteuzi huu unathibitishwa na maneno kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (8:28) kwamba: Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

Hongera sana.” Juzi Rais Samia alimpongeza Askofu Mkuu Mwandamizi Rugambwa kwa kuteuliwa kuwa Kardinali.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis alimteua Rugambwa kuwa Kardinali akiwa ni Mtanzania wa tatu kupewa jukumu hilo. Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima alisema Septemba 30, mwaka huu Papa Francis atampa majukumu rasmi ya ukardinali huko Vatican, Italia.

Askofu Mkuu Mwandamizi Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 Bunena-Bukoba. Alipata upadri Septemba 2, 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara. Aprili 13, mwaka huu, Papa Francis alimteua kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.

Juni 25, mwaka huu baada ya waumini kumpokea jimboni humo Askofu Mkuu Mwandamizi Rugambwa alimshukuru Mungu kwa neema ya wito wa kumtumikia akiwa padre na askofu.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button