MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Siku ya Amani Duniani Septemba 21 Jijini Dar es salaam lililoandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) yenye lengo la kuiombea nchi kutokana na mambo mabaya yanayoendelea ya utekaji.
Mwenyekiti wa JMAT Sheikh Alhad Mussa Salum amesema hayo ofisini kwake Dar es Salaam leo Septemba 18 wakati wa Mkutano na waandishi wa habari Ofisini.
Alhad amesema Kongamano hilo litahudhuriwa na zaidi ya wananchi 2,000 na miongoni mwa masuala watakayoyazungumzia ni pamoja na mambo yanahusu utaifa, mahusiano kama watanzania na udugu.
“Sisi kama viongozi wa dini letu ni kumuomba Mungu ili asaidie kumsaidia Rais na asaidie kuondosha mabalaa haya ambayo tuliyonayo ni kongamano muhimu sana la watanzania kujitokeza hasa viongozi wa dini kama tunavyojua amani ni jambo kubwa sana amani ndio kila kitu amani ndio maendeleo, amani ndio msingi unaomfanya mwanadamu kuweza kufanya mambo yake kwa mustakabadhi wa maisha yake,” amesema.
SOMA: Jumuiya ya Maridhiano wamualika Rais Samia
Amesema kwa pamoja tunaweza kuhakikisha kwamba utaifa unaendelea kudumu na watanzania wanaendelea kuimarisha umoja wao na kwamba kutofautiana ndio maisha na ndio maumbile yai wanadamu.
Kongamano hilo litahudhuriwa na viongozi mbalimbali kama Mabalozi, viongozi wa dini, wananchi ,viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, watu mashuhuri mbalimbali na wadau wengine.
Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania ni Jumuiya ambayo inawaleta pamoja watu wa dini zote na mila mbalimbali kwa ajili ya kutatua migogoro, kuleta umoja, amani na utangamano.