RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali inatekeleza kwa vitendo dhana ya mapinduzi ya kiuchumi kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kupambana na umasikini.
Amesema hadi sasa imeshatoa mikopo ya Sh bilioni 35.2 kwa wananchi 24,111.
Alisema hayo jana visiwani Zanzibar kwenye hotuba yake katika Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Leo Dk Mwinyi ataongoza maelfu ya wananchi katika uwanja wa Gombani kuhitimisha sherehe za miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar yenye kaulimbiu ‘Miaka 61 ya Mapinduzi, Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo Yetu’
“Kwa lengo la kuleta mapinduzi ya kiuchumi, tunaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kupambana na umasikini, tumeshatoa mikopo ya thamani hiyo kwa wananchi 24,111 wakiwemo wenye ulemavu 373,” alisema Dk Mwinyi.
Alisema mikopo hiyo imetolewa kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, kazi za mikono, ujenzi, kilimo na ufugaji na kuwa katika wanufaika hao asilimia 40 ni vijana.
Kadhalika, serikali imetoa Sh bilioni 60 kunufaisha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na kuwa katika kuwapatia mazingira bora ya kufanyia shughuli zao ujenzi wa masoko makubwa ya Mwanakwerekwe na Jumbi umekamilika na kuzinduliwa Novemba 2024.
Alisema kukamilika kwa masoko hayo, kumewawezesha zaidi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo 7,000 kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri na ya kudumu.
“Napenda kuwajulisha wananchi kuwa Soko la Chuini pamoja na kituo cha mabasi kilichopo katika eneo hilo, tunatarajia kulifungua mapema mwaka huu,” alisema.
Alisema serikali imeendelea na ujenzi wa masoko madogo katika mikoa na wilaya zote Unguja na Pemba ili kuepuka kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.
Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua za kuvutia wawekezaji na kutangaza fursa zilizopo katika maeneo ya Bandari Jumuishi ya Mangapwani huku ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme kwa ajili ya maeneo ya uwekezaji ukiendelea.