Dk Mwinyi amshukuru Bakhresa kwa uwekezaji

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameishukuru na kuipongeza kampuni ya Said Salim Bakhresa kuwekeza Dola za Marekani milioni 253.3 sawa na Sh bilioni 595 Zanzibar. Dk Mwinyi alitoa pongezi hizo wakati anazindua boti ya Kilimanjaro VIII inayomilikiwa na kampuni ya Azam Marine.

Uwekezaji huo uliochangia kukua kwa uchumi wa Zanzibar, umeiwezesha kampuni hiyo kupewa cheti cha uwekezaji wa kimkakati kitakachowapa fursa ya kupata punguzo la kodi katika baadhi ya maeneo. Dk Mwinyi alipongeza kampuni hiyo kwa kuona umuhimu wa kuwekeza Zanzibar na kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza uchumi wa buluu.

“Nawapongeza kwa kuendelea kuunga mkono serikali kwa kuzitumia fursa mbalimbali za uwekezaji, kama ilivyoelezwa kampuni hii ndiyo wawekezaji wakubwa hapa Zanzibar, mtaji waliowekeza tayari umeshavuka milioni 250 dola ni uwekezaji mkubwa na ninawapongeza sana,” alisema.

Advertisement

Dk Mwinyi alisema kampuni hiyo imeonesha uzalendo kwa kuwa ingeweza kuwekeza sehemu nyingine lakini ilitambua umuhimu wa kukuza uchumi wa Zanzibar. Alisema kampuni ya usafiri majini, Azam Marine ina mchango katika kukuza uchumi wa buluu uliogawanyika katika maeneo sita ukiwamo utalii.

Alitaja eneo lingine ni sekta ya usafiri na biashara baharini ambayo kampuni hiyo inaishikilia kwa asilimia kubwa kutokana na kumiliki vyombo vya usafiri wa baharini.

Aidha, alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni binafsi kuimarisha sekta ya usafiri wa majini sambamba na kuchukua hatua za kuboresha bandari kwa lengo la kuona usafiri wa majini unaendelea kuwa salama.

Pia alisema kuhusu ufinyu wa eneo la abiria katika bandari ya Malindi serikali ina mpango wa kujenga eneo lingine lakini ameagiza Mamlaka ya Bandari Zanzibar iangalie namna ya kuongeza eneo katika Bandari ya Malindi kwa muda wakati serikali inatafuta suluhisho la kudumu.