RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametoa miezi mitatu kwa wote waliopewa visiwa vidogo kuviendeleza na hawajafanya hivyo, waviendeleze vinginevyo baada ya muda huo serikali itavichukua na kuwapa wawekezaji wengine.
Alitoa agizo hilo jana Mjini Magharibi,Unguja wakati akimkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kufungua mradi wa Hoteli ya Cocoon Collection katika Kisiwa cha Bawe.
Kisiwa cha Bawe ni moja ya visiwa vidogo 16 vilivyopata wawekezaji na kuendelezwa kati ya visiwa 52 ambavyo Serikali ya Zanzibar imevitoa kwa ajili ya kukodishwa na kuendelezwa kwa uwekezaji.
“Natoa miezi mitatu wale wote waliopewa visiwa na hawajafanya chochote tutavichukua na tuwape wengine, tunataka kuona visiwa hivyo vinaendelezwa na si kubaki vilivyo,” alisema Dk Mwinyi.
Alisema mwekezaji Hotel ya Cocoon Collection aliyekodishiwa Kisiwa cha Bawe amefanya vizuri na ndani ya muda mfupi amekamilisha uwekezaji wa hoteli hiyo inayotajwa kutoa ajira zaidi ya 400 kwa Watanzania na kuchangia mapato ya serikali.
Dk Mwinyi alisema mbali na mwekezaji huyo kutoa ajira na kufanya uwekezaji huo mkubwa, pia ameendelea kusaidia wavuvi waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi eneo hilo kwa kuwajengea diko la kisasa eneo hilo la Bawe.
“Mbali na uwekezaji uliofanywa hapa, pia mwekezaji huyo amewajengea diko la kisasa wavuvi waliokuwa eneo hili na ameenda mbali zaidi, samaki wote wanaovuliwa na wavuvi hao wanawauzia hapo hotelini wanapata soko,” alisema Dk Mwinyi.
Alisema uwekezaji huo unakuza pia sekta ya utalii kwani Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020/2025 inaitaka Zanzibar kwenye eneo la utalii iongeze idadi ya vitanda kwenye utalii kutoka 10,000 hadi 15,000 ifikapo 2025.
Alisema idadi hiyo imefikiwa hata kabla ya muda tajwa kwani hivi sasa idadi ya vitanda kwenye hoteli za kitalii imeongezeka hadi kufikia vitanda 15,132.
“Hizo ni faida za uwekezaji bila kusahau ajira na tunategemea ajira zaidi zitakuja, hivyo Wazanzibari tusome tuwe na weledi kuchangamkia fursa sekta ya utalii,” alisema Dk Mwinyi.
Alisema Serikali ya Italia imesema itatoa Euro milioni 500 kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wanzanzibari waweze kuajirika kwenye sekta za hoteli za kitalii visiwani Zanzibar.