Dk. Mwinyi : Kombe libaki Tanzania

ZANZIBAR : RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameonesha uzalendo na mshikamano kwa klabu ya Simba SC kwa kuahidi kuhudhuria fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco, itakayopigwa Mei 25, 2025 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Ikulu ya Zanzibar, iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Raqey Mohamed, Rais Mwinyi ataungana na maelfu ya Watanzania kutoa sapoti kwa wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobaki kwenye michuano ya kimataifa.

“Uwepo wa Rais Mwinyi katika fainali hiyo unaashiria mshikamano mkubwa na unatarajiwa kuwa chachu ya ushindi kwa kikosi cha Simba,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa Morocco, Simba walifungwa mabao 2-0, hivyo wanahitaji ushindi wa angalau mabao 3-0 ili kutwaa taji hilo la heshima barani Afrika.

Aidha, Rais Mwinyi ametangaza kugharamia matumizi yote ya Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya fainali hiyo, kama zawadi maalum kwa Simba SC. Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuhamasisha ushindi na kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini.

“Uamuzi huu wa Rais Mwinyi unalenga kuonyesha mapenzi yake kwa michezo na kuhamasisha ushindi wa Simba kwenye mechi hii ya kihistoria,” ilieleza taarifa ya Ikulu.

SOMA: Mafanikio Simba yachomoza bungeni

Fainali hiyo inatarajiwa kuvuta mashabiki wengi kutoka ndani na nje ya nchi, huku matumaini yakiwa juu kwa Simba kutengeneza historia mpya kwa soka la Tanzania.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa itaendelea kuwa bega kwa bega na wadau wa michezo katika kuinua vipaji na kuipa soka ya Tanzania heshima kimataifa.

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button