KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewasili nchini Namibia akiongoza ujumbe wa CCM kwenye mazishi ya aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Namibia, Dk Sam Nujoma Machi Mosi, mwaka huu.
Dk Nchimbi aliwasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Hosea Kutako jijini Windhoek juzi.
Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Caesar Waitara alimpokea kiongozi hiyo akiwa amefuatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid.
Balozi Nchimbi alitarajiwa kushiriki ratiba za kutoa heshima za mwisho na kumuaga Dk Sam Nujoma kuanzia jana.
Chama tawala cha Namibia, SWAPO ambacho ni rafiki wa kihistoria wa CCM kimeandaa shughuli kwa ajili ya heshima ya muasisi wake huyo.
Katika hatua nyingine, leo Dk Nchimbi atashiriki ibada ya kitaifa ya kumuaga Nujoma na shughuli ya maziko ya kitaifa itafanyika Machi Mosi katika eneo la makaburi ya mashujaa yaliyoko makao makuu ya nchi hiyo jijini Windhoek.
Uhusiano kati ya Namibia na Tanzania halikadhalika CCM na SWAPO na watu wa nchi hizo mbili ni wa kihistoria tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru dhidi ya wakoloni na makaburu.
Dk Nujoma na viongozi na wanachama wengi wa SWAPO na Namibia waliishi uhamishoni nchini Tanzania tangu miaka ya 1960 wakishiriki mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao.
Walianzisha chama cha SWAPO nchini ili kuendesha shughuli za kuikomboa nchi yao kisiasa hadi walipopata uhuru mwaka 1990.