Dk Nchimbi: Msikubali kufarakanishwa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amewataka watanzania wasimame kidete kukataa kufarakanishwa na maneno ya wanasiasa.

Badala yake amewasisitiza kusimamia mambo yaliyo ya msingi yenye manufaa kwao na taifa kwa ujumla, huku akipongeza wana CCM kwa kufanya kampeni kwa kuzingatia utulivu na amani.

Dk Nchimbi ameeleza hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Mbagala lililopo wilayani Temeke Dar es salaam akihitimisha mikutano ya kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika leo Novemba 27, 2024.

Advertisement

Alisema vyama mablimbali vya siasa vilijitokeza kuomba nafasi mbalimbali zinazowaniwa katika katika mitaa 80,400 nchi nzima na kusisitiza CCM imeweza kuweka watu 49,000 ambao ni sawa na asilimia 61 ya watanzania watakaopigiwa kura za ndio na hapana.

Aliongeza kwa wapinzani imekuwa pungufu ya kwao kwani waliweza watu takribani 30,000 tu.

Pia alisema wakati wa kupiga kura za maoni jumla ya watu 356,000 waliomba kupitishwa huku watu 80,000 walifanikiwa kupita lakini asilimia 99 ya walioshinda kura za maoni ndio walioteuliwa kuwania nafasi katika uchaguzi huo.

Aliongeza zaidi ya watu ambao hawakuteuliwa kulikuwa na sababu mbalimbali ikiwemo kutokukomaa kisiasa na wengine walipendwa sana na wananchi lakini hawakupata nafasi kwakuwa hawakujua kusoma na kuandika.

Alisisitiza kuwa mbali na watu zaidi ya 280,000 kutoteuliwa lakini wameonyesha ushirikiano mkubwa na kuwaunga mkono wenzao walioteuliwa kuhakikisha CCM inashinda katika uchaguzi huo.

Alisema vyama vyotevya siasa vinatimiza jukumu la kidemokrasia kwenda kwenye uchaguzi lakini ni hiari ya mtanzania kuchagua chama kitakachoweza kuwawakilisha vizuri, kisichopenda ugomvi, kinatetea na kuona fahari kutumikia wananchi na kina kiu ya maendeleo.

Aidha Dk Nchimbi alisisitiza wana CCM kujizuia na kujiepusha na kuacha kugombana gombana kwani kunapoelekea chama kupoteza imani ya wananchi na kudharaulika hasa katika kipindi cha uchaguzi.

“Watanzania katika mikutano ya hadhara wanawez awakakupigia makofi lakini wakitoka wanaenda kusimuliana na kukudharau, wanakupigia makofi lakini kura wanakunyima,” alisema Dk Nchimbi.

Alisema CCM imepimwa vya kutosha na wananchi na wameona kuwa kinafaa kuwaongoza, hivyo amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.