Dk Shein: Vijana jengeni mitandao ya kitaaluma

DAR ES SALAAM: MKUU wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye pia ni Rais mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, amewataka wahitimu wa chuo hicho pamoja na vijana nchini kujenga mitandao imara ya kitaaluma na kuendelea kulinda amani na mshikamano wa taifa, akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa mafanikio yao ya sasa na baadaye.

Akizungumza katika mahafali ya Ndaki ya Dar es Salaam, Dk  Shein alisema wahitimu hawapaswi kusubiri fursa kutafutiwa bali wanapaswa kuanzisha na kuimarisha mahusiano ya kitaaluma yatakayowaunganisha na dunia ya ajira na utafiti.

Alitaja mfano wa wanafunzi wa sheria waliowakilisha chuo katika mashindano ya kimataifa ya Mahakama Igizi Mjini Vienna, Austria, akisema yalitoa nafasi ya kujifunza utaalamu, tamaduni na kuunda mitandao ya kimataifa.

Katika hotuba yake, Dk Shein pia alizungumzia umuhimu wa kulinda amani, akibainisha kuwa amani na mshikamano ndio nguzo kuu zinazowawezesha vijana kufikia malengo yao. “Katika mazingira ya sasa yenye ushindani wa elimu na ajira, hakuna maendeleo yatakayopatikana bila kuwepo amani. Lazima tuilinde kama tunavyolinda maisha yetu,” alisema.

Aidha, alitaka kufanyika kwa utafiti kubaini chanzo cha wanafunzi wa sheria kukosa nafasi za mafunzo kwa vitendo, na endapo ratiba za chuo zinahitaji kurekebishwa, hatua zichukuliwe ili kuwawezesha kupata nafasi hizo kwa wakati.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, alisema Ndaki ya Dar es Salaam ina jumla ya wanafunzi 1,793 ambapo wanawake ni asilimia 52.4, akisema ongezeko hilo linaonyesha mwamko mkubwa wa wanawake katika kujiendeleza kielimu. Alibainisha kuwa Ndaki imeendelea kutoa huduma kwa jamii kupitia semina na mafunzo, ikiwemo kuwawezesha wanawake wa Tegeta kufahamu matumizi ya Baraza la Usuluhishi la Kata na kutoa elimu ya masoko kwa wafanyabiashara wa ice cream katika maeneo ya Magomeni, Kigamboni na Chanika.

Prof. Mwegoha aliongeza kuwa chuo kinaendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufanyia kazi, ikiwemo ukarabati wa majengo, ujenzi wa vimbweta, maboresho ya TEHAMA na ujenzi wa jengo la taaluma lenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 ambalo tayari limefikia asilimia 15 ya ujenzi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahya-Othman, aliwahimiza wahitimu kuitumia elimu waliyoipata kuchochea mabadiliko chanya katika jamii, huku Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashimu Abdallah, ambaye pia ni mhitimu, akisema elimu aliyoipata itamuwezesha kutatua changamoto za wananchi anaowaongoza.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wazazi, wahadhiri na wanafunzi, ambapo wahitimu walihamasishwa kuwa mabalozi wa amani, maadili na maendeleo ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button