Dk Slaa atoa msimamo siasa ya vyama

DAR ES SALAAM; ALIYEWAHI kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Wilbroad Slaa amesema hatorudi kwenye siasa ya vyama.

Dk Slaa alitoa msimamo huo jana asubuhi alipozungumza katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds cha Kampuni ya Clouds Media ya Dar es Salaam.

Alisema tangu alipoondoka Chadema mwaka 2015, hajajiunga na chama chochote na kwa miaka karibu mitatu tangu arudi nchini amekuwa akifanya kazi ya kulea vizazi na kuwaongoza namna ya kufanya siasa nzuri na safi.

Advertisement

“Nafanya kazi kupitia kundi linaitwa Sauti ya Watanzania kupitia njia ya mtandao na kwa ujumla lina watu kama 3,000 kwa sababu mimi naamini katika kulea vizazi kuandaa vijana waje wachukue nafasi mbalimbali kwa siasa nzuri na si siasa safi,” alisema Dk Slaa ambaye pia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.

Alisema aliamua kuondoka Chadema kwa kuwa alikuwa na misimamo tofauti kuhusu jambo waliloamua kufanya la kumleta mgombea ambaye yeye aliamini hakufaa kuwa kiongozi.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/dk-slaa-avuliwa-hadhi-ya-ubalozi/

“Kwa mwanasiasa yeyote makini anajua kwamba mkienda tofauti na kwa kuwa chama kinakuwa na sera, falsafa na mipango mbalimbali ambayo mlikuwa mmekubaliana na wenzako badala ya kuleta vurugu wewe ambaye uko tofauti unakaa pembeni…kwa hiyo mimi niliamua nikae pembeni,” alisema Dk Slaa.

Pia alisema baada ya kumaliza muda wake wa ubalozi nchini Sweden na kurudi nchini, aliwahi kuitwa kwa ajili ya kupewa nafasi ya uongozi katika bodi mojawapo kati ya bodi za serikali, lakini alikataa na akawaeleza wahusika kuwa ni muda wa yeye kupumzika.

Akizungumzia kuhusu ukomo wa uongozi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema wanaozua mijadala ya suala hilo ni wabaya wa Mbowe wanaotaka kumuondoa.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/mtaturu-dk-slaa-amepoteza-mwelekeo/

“Wakati sisi tunaingia kwenye vyama kumpata mgombea akishajionesha kuwa anaenda kugombea anachomewa nyumba kwa hiyo tulifikia hatua ya kuondoa ukomo ili tupate wale wajasiri na Mbowe haogopi tena mpaka leo,” alisema Dk Slaa.

/* */