DP WORLD, TEAGTL zaongeza mapato bandarini

DODOMA: SERIKALI imesema tangu kuanza ushirikiano na Kampuni ya DP World na Tanzania East Africa Gateway terminal limited (TEAGTL) katika Bandari ya Dar es Salaam kumefanikisha ongezeko la mapato yatokanayo na Kodi ya Forodha kutoka Sh trilioni 7.08 katika kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024 hadi kufikia Sh trilioni 8.26 katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la Sh trilioni 1.18.
Takwimu hizo zimebainishwa leo Mei 15, 2025 bungeni jijini Dodoma kwenye na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2025/26, akieleza pia gharama za uendeshaji wa bandari hiyo umepungua kutoka Sh bilioni 975.01 hadi kufikia Sh bilioni 685.16 sawa na punguzo la takribani asilimia 30.
SOMA ZAIDI: Uwekezaji DP World waanza kuleta matunda
“Mashirikiano na sekta binafsi yamesaidia pia kupungua muda wa kusubiri melu nangani kutoka wastani wa siku 46 hadi wastani wa siku saba kwa meli za mizigo mchanganyiko na kichele na meli za makasha gatini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku tatu,” amebainisha Prof Mbarawa.
Aidha, ameeleza kuwa faida nyingine ya ushirikiano huo ni pamoja na kuongezeka kwa wastani wa shehena ya makasha inayohudumiwa kwa mwezi, kutoka makasha 17,000 hadi makasha 25,000 sawa na Ongezeko la asilimia 47.
SOMA ZAIDI: DP World yamaliza foleni bandarini
“Mhe. Spika kwa ujumla hatua hii ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kuendeleza na kuendesha bandari nchini, umechanhia kufikiwa mapema kwa lengo la mpango kabambe wa TPA wa miaka 20 uliowekwa wa kuhudumua tani milioni 30 za shehena ifikapo mwaka 2029/30,” amesema Prof Mbarawa.
Amebainisha kwamva matokeo ya uendeshaji wa bandari hiyo hadi kufikia Machi 2025 tayari ufanisi wa uhudumiaji wa shehena zote nchini umefikia tani milioni 27.55 na kuwa kwa mwenendo uliopo lengo la tani milioni 30 litafikiwa mapema kabla ya muda uliowekwa katika mpango wa TPA.



