Waziri wa Sheria DRC kuhojiwa

DR CONGO : WAZIRI wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Constant Mutamba, anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya takriban dola milioni 20 za Marekani, ambazo zilikuwa zimekusudiwa kwa ajili ya kufidia waathirika wa vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa hizo zilitolewa jana na Spika wa Bunge la DRC, Vital Kamerhe, ambaye amesema kuwa bunge limeanzisha mchakato wa kumhoji Waziri Mutamba kupitia tume maalum ya uchunguzi, ambayo itaundwa na wabunge watakaotangazwa hivi karibuni.

“Tumeunda tume maalum ya kibunge kwa ajili ya kumhoji Waziri wa Sheria kuhusu tuhuma hizi nzito zinazohusu fedha zilizotengwa kwa fidia ya waathirika wa migogoro ya kijeshi mashariki,” alisema Kamerhe.

Kwa mujibu wa Spika huyo, hatua hiyo inalenga kuhakikisha uwajibikaji serikalini na kuthibitisha matumizi sahihi ya fedha za umma, hasa zile zinazolenga kusaidia wananchi waliokumbwa na madhila ya vita.

Wakati huo huo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, amenukuliwa akiwasilisha barua rasmi kwa bunge, akiomba kupigwa kwa kura ya kumuondolea Mutamba kinga ya ubunge, ili kuruhusu uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu madai ya ufisadi dhidi yake.

SOMA: M23 kuwaponza Waandishi wa Habari DRC

Iwapo kura hiyo itapitishwa, Mutamba atakabiliwa na uchunguzi rasmi na huenda akafunguliwa mashitaka mahakamani, jambo linaloweza kuwa mtihani mkubwa kwa serikali ya Rais Félix Tshisekedi katika vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Bunge linatarajiwa kutangaza rasmi majina ya wajumbe wa tume maalum, kabla ya hatua ya upigaji kura kufanyika ndani ya siku chache zijazo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button