DRC yakubali kutuma ujumbe Angola

DR CONGO : SERIKALI ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imepanga kutuma ujumbe nchini Angola Jumanne hii kwa ajili ya kufanya mazungumzo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, katika juhudi za kutafuta suluhu la mzozo unaoendelea Mashariki mwa nchi hiyo.

Mazungumzo haya, ambayo yatafanyika mjini Luanda, yamepangwa kuanza tarehe 18 Machi, na yanatarajiwa kuwa ya moja kwa moja kati ya Serikali ya DRC na waasi wa M23. Wiki iliyopita, Serikali ya Angola ilitangaza kuwa itakuwa mwenyeji wa majadiliano hayo, lengo kuu likiwa ni kuleta amani na kumaliza mapigano yanayoendelea.

Rais Felix Tshisekedi awali alikataa kufanya mazungumzo na M23, lakini baadaye alibadili msimamo wake na kuonyesha utayari wa kukutana nao. Hata hivyo, msemaji wa Rais, Tina Salama, alisema kuwa hadi sasa bado haijajulikana ni nani atakayekuwemo katika ujumbe wa DRC katika mazungumzo hayo.

Kundi la waasi la M23 kupitia msemaji wao, Lawrence Kanyuka, limethibitisha kupokea mwaliko kutoka Angola, ingawa hawajathibitisha kama watashiriki kwenye mazungumzo hayo. M23 imeitaka Serikali ya DRC, chini ya Rais Tshisekedi, kueleza hadharani dhamira yake ya kutaka mazungumzo ya moja kwa moja.

Serikali ya Angola imekuwa ikijitahidi kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo huu, huku ikijaribu kupunguza mvutano kati ya DRC na Rwanda, inayoshutumiwa kwa kuunga mkono M23. Hadi sasa, Rwanda imeendelea kukanusha tuhuma hizo.

SOMA: DR Congo yakanusha kukamatwa FDLR

Kwa upande mwingine, mzozo huu umesababisha vifo vingi katika eneo la Mashariki mwa DRC. Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu 1,500 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa mapigano haya, huku mamia ya wengine wakiwa wamejeruhiwa na zaidi ya watu 500,000 wakikimbia makazi yao kutokana na machafuko hayo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button