WIKI iliyopita, viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walifanya mkutano wa pamoja Dar es Salaam kuzungumzia utatuzi wa mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Huu ni mkutano ulioonesha nia thabiti ya nchi wanachama wa jumuiya hizo katika kutafuta Suluhu ya kudumu ya nchi hiyo ambayo mgogoro wake unatia doa ukanda mzima wa Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika.
SADC na EAC wameonesha nia thabiti ya kutaka kujenga heshima ya ukanda kwa kujitoa bila kujali mazingira ya
mgogoro, kwa nia ya kuhakikisha amani inapatikana DRC.
Ipo methali ya Kiswahili isemayo; ‘Penye nia pana njia’ ambayo inatuongoza kuamini kwamba nia iliyooneshwa na
nchi hizi, itatoa njia kwa maana ya kusaidia kuleta utulivu.
Ni matumaini yetu kwamba nchi wanachama wa SADC na EAC zitajitoa ipasavyo bila kuchoka, kukata tamaa na hata
bila kujali ukinzani wowote ule katika mgogoro wa DRC.
Tunategemea wanajumuiya hawa watafuata nia yao ya dhati kudhihirishia dunia kwamba nchi za Afrika zinao uwezo wa kuzungumza, kushauri na kufikia muafaka hata katika mazingira yanayodhaniwa kuwa ni vigumu kupata suluhisho.
Siku zote kusudi au dhamira ikiwepo kuhusu jambo lolote, kwa vyovyote vile njia ya kufanikisha itapatikana. Vivyo
hivyo asiyekuwa na nia au kusudi hawezi kuchukua hatua!
Tunapongeza umoja huu wa SADC na EAC tukiamini katika mantiki ya kwamba penye wengi hapaharibiki neno kwa maana kwamba, fikra na nguvu zao zitafanikisha kurejesha amani ya DRC.
Tuna imani nguvu na umoja huu hautatetereka kama ambavyo wamenukuliwa viongozi wa SADC na EAC kwa
nyakati tofauti wakiahidi kutorudi nyuma.
Mathalani, Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa alinukuliwa akisema mkutano huo wa
pamoja ni ushuhuda wa umoja wao katika nia yao ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa DRC.
Hatuna shaka na busara na juhudi za nchi hizi katika kuleta amani, upatanisho na kumaliza mgogoro DRC.
Aidha, ni wakati wa pande zinazokinzana DRC kuweka silaha chini na kuruhusu meza ya mazungumzo kama ilivyoshauriwa na Mwenyekiti wa EAC, Rais wa Kenya, William Ruto. Pasiwepo msafihi katika mchakato huu wa kuleta amani ya kudumu.
Kiuhalisia, wanaoumia ni raia wa kawaida ambao wameshuhudiwa wakikimbia machafuko, wengine wakikabiliwa na
ukatili na hata kuuawa hususani wanawake na watoto.
Tunazidi kupongeza nia hii ya kumaliza mgogoro hasa kwa nchi wanachama kuazimia pia kuhusisha pande zote,
kuangalia chimbuko la mgogoro na kuja na mapendekezo ya suluhu.