HALI ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) bado iko kutokana na matukio ya ukosefu wa usalama, mapigano ya ndani na machafuko yanayoendelea yakiathiri maisha ya mamilioni ya watu.
Tunatoa pole nyingi kwa Serikali ya Tanzania kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kupoteza askari wake wawili kutokana na mashambulizi ya waasi wa M23, Januari 24 na 28, mwaka huu.
Askari hao waliungana na walinda amani chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika mashariki mwa DRC (SAMDRCS). Vifo vya askari hao na wa nchi nyingine ni uthibitisho kwamba machafuko hayo yana athari kubwa pia kwa majirani hususani EAC.
Katika mazingira hayo, ni muhimu kwa nchi wanachama kuungana, kuendelea kuimarisha juhudi za kutafuta amani ya kudumu nchini DRC.
DRC ni nchi yenye rasilimali nyingi, lakini ukosefu wa usalama unaofanywa na vikundi vya waasi na migogoro ya kisiasa unachangia kwa kiasi kikubwa kudumaza maendeleo yake.
Tunatambua ambavyo nchi za EAC zimekuwa zikibeba jukumu la kutaka kuleta amani nchini humo bila kusahau mkutano wa viongozi wakuu wa nchi wanachama uliofanyika Desemba mwaka jana kujaribu kuleta amani mashariki mwa DRC lakini bila mafanikio.
Vilevile, mkutano wa hivi karibuni wa wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya uliofanyika kwa njia ya mtandao, jumuiya ilitoa wito kwa DRC kufanya mazungumzo na pande zote zinazohusika na mzozo wa mashariki mwa nchi hiyo wakiwemo M23.
Huu ni uthibitisho kwamba jumuiya inaguswa na hali hii huku ikitamani kuona amani inapatikana. Ndiyo maana tunasisitiza EAC isichoke.
Pia, iendelee kusaidia kuleta uthabiti wa amani na usalama katika eneo hili kwa kuzingatia kwamba nchi moja inapokuwa katika hali tete, ni wazi majirani wote hawawezi kukwepa athari zake.
Hivyo basi, litakuwa ni jambo la busara kwa nchi za EAC kuendelea na mchakato wa kidiplomasia wa kujenga amani, kwa kushirikiana na jamii ya kimataifa,
ili kuweza kuleta suluhu la kudumu katika mzozo huu. Tuna imani kwamba nchi wanachama hazijachoka kusaidia kuondoa nguvu zinazochochea migogoro DRC na kuimarisha mshikamano katika jamii.
Ni muhimu wasichoke katika juhudi zao, kwa sababu amani ya DRC ni muhimu si tu kwa watu wa nchi hiyo bali pia kwa utulivu wa kikanda.
Mshikamano na uhamasishaji wa pamoja utawezesha kuleta mabadiliko chanya na kuifanya DRC kuwa mahala salama na penye maendeleo kwa maslahi ya ukanda na Afrika kwa ujumla.