ARUSHA: J UMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kushirikiana na Internet Society Tawi la Uganda, watakuwa wenyeji wa Jukwaa la 11 la Utawala wa Mtandao wa Afrika Mashariki (EAIGF) Septemba mwaka huu.
Jukwaa hilo litafanyika Septemba 11 hadi 12 mjini Kampala nchini Uganda chini ya kaulimbiu isemayo ‘Kujenga Mustakabali wetu wa Kidijitali wa Wadau kwa Afrika Mashariki’.
Taarifa ya hivi karibuni ya Ofisa Mwandamizi Idara ya Mawasiliano ya Umma na Masuala ya Umma, Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Arusha, Simon Owaka kwa vyombo vya habari, ilisema kuwa lengo la msingi la EAIGF ni kuunda jukwaa jumuishi la majadiliano la kimataifa la wadau wa lugha mbalimbali.
Akizungumzia jukwaa hilo, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Sekta za Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa, Andrea Malueth aliwataka wadau wa sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa kanda na wadau wengine kutumia jukwaa hilo kuunda ajenda ya ushirikiano wa kidijiti.
“Katika hali ya kidijitali inayoendelea kwa kasi, utawala bora wa mtandao ni muhimu kwa ajili ya kukuza uvumbuzi, usalama na kukuza ushirikishwaji.Kama EAC, tumedhamiria kujenga mustakabali wa kidijitali wa wadau mbalimbali ambapo serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wasomi watashirikiana vyema,” alisema Malueth.
Amesema kupitia ushirikiano huo pekee ndipo EAC itaweza kuunda Afrika Mashariki iliyounganika zaidi na yenye ustawi katika ujuzi, miundombinu thabiti na upatikanaji sawa wa fursa za kidijiti.
“Juhudi zetu za pamoja zitawawezesha wananchi wetu kuimarisha ukuaji wa uchumi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kutusukuma kuelekea mustakabali mzuri wa kidijitali,” alisema.
SOMA: SIKU YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI: Manufaa yake makubwa kisiasa, kiuchumi yatajwa
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tangu kuanzishwa mwaka 2008, EAIGF imetumika kama jukwaa muhimu la mazungumzo kuhusu masuala ya Utawala wa Mtandao katika Afrika Mashariki ambalo linakuza mtazamo wa wadau unaoleta pamoja wawakilishi kutoka serikalini, vyombo vya habari, sekta binafsi, asasi za kiraia na wasomi ili kuunda mustakabali wa mtandao katika kanda hiyo.