EAC yatenga mamilioni ya fedha kukuza Kiswahili

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imeitengea Tume ya Kiswahili Afrika Mashariki (EAKC) Dola za Marekani 1,502,535 (takribani Sh 3,584,736,742 za Tanzania) katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24 kuiwezesha kupanga na kutekeleza malengo yake. Aidha, EAKC imefadhili wanafunzi watano wa shahada ya uzamili kufanya utafiti wa Kiswahili katika nchi wanachama wa EAC.

Taarifa ya Sekretarieti ya EAC kwa HabariLEO Afrika Mashariki, ilisema hayo yalibainika wakati Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Afrika Mashariki, Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi, Dk Ezechiel Nibigira, akiwasilisha hotuba ya bajeti EAC kwa Mwaka wa Fedha wa 2023/24 katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Mbali na EAKC, Dk Nibigira alitaja bajeti iliyotengwa na EAC kwa taasisi na mashirika yake mengine na kiasi cha Dola kwenye mabano kuwa ni Sekretarieti ya EAC (Dola 50,931,553), Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (Dola 4,450,488), Bunge la Afrika Mashariki (17,681,365) na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (Dola 8,471,980).

Mashirika na taasisi nyingine za EAC ni Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki (Dola 2,016,543), Tume ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki (Dola 2,193,811), Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki–EACA (Dola 1,391,667), Shirika la Uvuvi wa Ziwa Victoria (Dola 2,807,993) na Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki-IUCEA (Dola 12,394,945). Kuhusu utafiti wa Kiswahili EAC, Dk Nibigira aliliarifu bunge hilo kuwa, wanafunzi hao walifadhiliwa na EAKC katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23.

Alisema katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24, EAKC itazingatia uundaji wa sera ya lugha ya Kiswahili ili kuwezesha maendeleo na matumizi ya Kiswahili katika nyanja rasmi kuadhimisha Siku ya Pili ya Kiswahili Duniani na kufanya Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili.

“Aidha, tume itazingatia na kujikita kutafsiri na kufasiri ala za EAKC kwa Kiswahili ili zitumike katika shughuli rasmi,” alisema. Akizungumzia mafanikio yaliyotekelezwa katika mwaka huu wa fedha utakaomalizika Juni 30, Mwenyekiti huyo alisema: “Tume ya Kiswahili Afrika Mashariki iliratibu uundaji wa mipango ya kitaifa ya utekelezaji wa kupitishwa kwa Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Jumuiya na kufanikisha uzinduzi wa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani Zanzibar, Tanzania.

” Alisema uzinduzi huo ulikuwa matokeo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2021 kuteua na kuitangaza Julai 7, kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani kwa kutambua umuhimu wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano duniani.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button