Ekari 101 za bangi zateketezwa

Ekari 101 za bangi zateketezwa

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ( DCEA)  imeteketeza jumla ya ekari 101 za mashamba ya bangi sawa na kiasi cha kilo 550 za bangi mbichi.

Pia imeteketeza magunia  482 ya aina hiyo ya dawa za kulevya katika eneo la Kisimiri juu kata ya Uwalu, wilayani  Arumeru mkoani Arusha.

Ukamataji huo umefanyika kufuatia agizo la Rais Dk Samia Suluhu Hassan kufanya operesheni nchi nzima, ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini.

Advertisement

Taarifa iliyotolewa DCEA leo June Mosi, 2023 imesema kuwa  operesheni hiyo,imeongozwa na  Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo,  Aretas Lyimo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na  usalama.

Lyimo amesema kuwa DCEA  itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo hayo, ili kuhakikisha bangi inatokomea kabisa mkoani humo na hatimaye  wakulima na wananchi  kwa ujumla wanaoishi katika eneo la Kisimiri juu na chini wanaachana na kilimo cha bangi na kujikita katika mazao mengine ya biashara badala ya bangi.

Amesema, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa  katika kuhakikisha agizo la Rais linatekelezwa, ameelekeza kufanyika kwa utafiti kujua ni mazao gani mbadala yanaweza kulimwa katika maeneo hayo ambayo yamekithiri kwa kilimo hicho cha bangi.

“Ili wananchi wa maeneo husika waweze kupewa mbinu mbadala za kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara badala ya kuendelea na kilimo cha bangi, tumewasiliana na Wizara ya Kilimo na ofisa kilimo wa kata ya Uwalu hapa Kisimiri, ambaye ameeleza tayari utafiti huo umefanyika,” amesema.

Naye,  Ofisa Kilimo,  Samwel Palangyo, amesema kuwa, utafiti uliofanywa na Wizara ya Kilimo kupitia kituo cha utafiti  wa kilimo cha TARI Tenguru, imebaini kuwa  yapo mazao yanayostawi katika maeneo hayo kama vile  pareto, karoti na viazi mviringo na kuwa mbadala wa zao haramu la bangi ambalo halifai katika jamii.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *