EMCA Yasistiza utunzaji mazingira

DAR ES SALAAM: Taasisi ya EMCA, inayojihusisha na utunzaji wa mazingira na utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo, imeendelea na kampeni yake ya “Tuelimishe Mazingira” kwa kutembelea Shule ya Msingi Mlimani Demonstration jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa EMCA, Zafarani Ramadhani, alisema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha jamii, hususan watoto, kutambua wajibu wao katika kuhifadhi mazingira na kuhakikisha maeneo yao yanabaki salama na safi.

Katika shughuli hiyo, Taasisi ya EMCA ilitoa vitendea kazi vya usafi ikiwemo mafagio, vifaa vya kuhifadhi taka, pamoja na kushiriki zoezi la upandaji miti baada ya kutoa darasa juu ya umuhimu wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Mlimani Demonstration, Florence Karara, aliishukuru taasisi hiyo kwa msaada na elimu waliowapatia, akibainisha kuwa vitendea kazi hivyo vitachangia kwa kiasi kikubwa kuweka mazingira ya shule katika hali ya usafi na kuimarisha afya za wanafunzi.
“Upandaji miti unaleta vivuli na hewa safi, na usafi shuleni unawasaidia wanafunzi kujifunza katika mazingira rafiki,” alisema.

Naye mmoja wa wanafunzi wa darasa la saba, Avoidance Mwanzo, alisema mazingira safi yanaboresha uwezo wa mwanafunzi kujifunza na hatimaye kuongeza ufaulu.
“Mazingira safi yanatupa utulivu na hamasa ya kusoma vizuri,” alisema.

Mwisho, walimu na wanafunzi walitoa wito kwa taasisi na wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuunga mkono jitihada za utunzaji mazingira na kutoa vifaa vitakavyowezesha shule kuendeleza utamaduni wa usafi na uhifadhi wa mazingira.



