Eng. Rose Mayembe: Sauti ya Tanzania Kimataifa katika Sekta ya Madini

KATIKA juhudi za Tanzania kuendelea kujitangaza kimataifa kupitia sekta ya madini, wanawake wa Kitanzania wameendelea kung’ara katika majukwaa mbalimbali ya madini barani Afrika na duniani. Hivi karibuni, katika Kongamano la African Mining Indaba lililofanyika nchini Afrika Kusini, Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wanawake Afrika (AWIMA) lilitoa tuzo kwa wanawake waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya madini barani Afrika.

Katika tuzo hizo, wanawake wawili kutoka Tanzania waliibuka washindi katika vipengele tofauti. Miongoni mwao ni Mhandisi Rose Mayembe, aliyeshika nafasi ya pili katika kipengele cha Leading Woman in Large-Scale Mining in Africa. Nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mshindi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku nafasi ya tatu ikienda kwa mshindi kutoka Afrika Kusini.

Rose Mayembe ni nani?

Mhandisi Rose Mayembe ni mtaalamu wa masuala ya kimazingira na kijamii katika sekta ya madini, akijikita pia katika uchimbaji endelevu na masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Anasema safari yake katika sekta ya madini ilianza takribani miaka 12 iliyopita aliposhiriki katika utekelezaji wa hatua za kufunga na baada ya kufungwa kwa mgodi mkubwa wa dhahabu wa Golden Pride Project (GPP) uliokuwa unamilikiwa na kampuni ya Resolute Mining wilayani Nzega, mkoani Tabora.

Rose anasema uzoefu huo ulimfundisha umuhimu wa kuzingatia mipango ya kimazingira na kijamii mapema katika miradi ya madini ili kupunguza madhara kwa jamii na mazingira. “Hapo ndipo niliona umuhimu wa kuingiza fikra za mabadiliko ya tabianchi na ubunifu tangu mwanzo wa mradi,” anasema.

Tuzo ya Mining Indaba

Katika kongamano la Mining Indaba, Rose alitambuliwa kama mshindi wa pili wa tuzo ya Leading Woman in Large-Scale Mining in Africa. Anasema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwake na kwa Tanzania kwa kuwa majukwaa ya aina hiyo huwakutanisha serikali, wawekezaji, kampuni kubwa za madini na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Rose, ushindi huo unaonesha uwezo wa wanawake wa Kitanzania kushindana na kuongoza katika sekta ya uchimbaji mkubwa wa madini barani Afrika.“Kwa wanawake, tuzo hii ni ishara ya kuvunja vikwazo na kuthibitisha kuwa tunaweza kushiriki katika meza za maamuzi na kusukuma mbele ajenda ya madini yenye uwajibikaji na ushindani wa kimataifa,” anasema.

Mbali na tuzo hiyo, mwaka 2025 Rose alipokea Global Advocacy Award (GAA) katika kipengele cha Clean Energy and Sustainable Mining, tuzo iliyotolewa katika Global Advocacy Forum Awards (GAF 2025) jijini London, Uingereza. Tuzo hiyo ilitambua mchango wake katika kukuza malengo ya maendeleo endelevu, hususan SDG 7 inayohusu nishati safi na nafuu.

Safari yake katika sekta ya madini

Kwa sasa, Rose anashiriki katika miradi ya kitaifa na kimataifa inayohusisha hatua zote za maisha ya mgodi kuanzia usanifu wa mgodi, uendeshaji, kufungwa kwa mgodi hadi hatua za baada ya kufungwa. Anasema lengo lake ni kuhakikisha sekta ya madini inaleta mapato kwa taifa huku ikilinda mazingira, kuheshimu haki za binadamu na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii. “Nilipoanza kuzungumza kwa takwimu na maandalizi ya kitaalamu, niligundua kuwa uongozi si lazima uwe cheo, bali ni uwezo wa kuathiri maamuzi,” anasema.

Kilichomfikisha hapo alipo

Rose anasema mafanikio yake yametokana na uamuzi wa ndani wa kujiamini na kutokusubiri kuthibitishwa na wengine katika sekta ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume. “Nilitambua kuwa ubora wa hoja unazidi sauti ya anayezungumza,” anasema.

Anasema kinachomtofautisha ni uwezo wa kuunganisha taaluma mbalimbali katika mtazamo mmoja wa kimkakati, akitazama sekta ya madini kama mfumo unaogusa uhandisi, mazingira, jamii, uchumi na sera. Kwa mujibu wa Rose, uzoefu wake katika hatua zote za maisha ya mgodi umemwezesha kuona picha pana ya sekta na kutoa mapendekezo yanayozingatia uendelevu.

Wanawake katika sekta ya madini

Rose anasema wanawake katika sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji na wataalamu wanaoshiriki katika sekta hiyo, wanahitaji zaidi kuaminiwa na kupewa nafasi za uongozi. Anasema changamoto kubwa si uwezo bali ni fursa. “Tunahitaji kushirikishwa katika maamuzi ya kimkakati, bodi na sera badala ya kubaki katika utekelezaji pekee,” anasema.

Uchimbaji mdogo

Kuhusu sekta ya uchimbaji mdogo, Rose anashauri serikali na wadau kuanza kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwarasimisha, kuwawezesha kupata mitaji na kuwapatia elimu ya biashara pamoja na mafunzo ya mazingira na usalama. Anasema kuwepo kwa mwongozo rahisi wa tathmini ya athari za mazingira (EIA) na ufuatiliaji wa kitaalamu kunaweza kusaidia kuboresha sekta hiyo bila kuongeza mzigo wa kisheria kwa wachimbaji wadogo.

Wito kwa wanawake na wasichana

Rose anatoa wito kwa Watanzania, hususan wanawake na wasichana, kuona sekta ya madini kama fursa ya ubunifu na uongozi badala ya kuiona kama sekta ya jinsia fulani. “Jiwekezeni katika elimu na ujuzi, na msisite kushiriki katika meza za maamuzi. Uwezo hauna jinsia,” anasema.

Anaongeza kuwa madini ni chachu ya maendeleo, lakini maendeleo ya kweli yanapatikana pale wanawake na vijana wanaposhiriki kikamilifu katika sekta hiyo. “Naamini kizazi kijacho cha wanawake hakitaomba nafasi, kitakuwa sehemu ya mwelekeo wa sekta hii,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button