“Epukeni kuwaweka watu kwenye foleni ndefu”

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amewaagiza maofisa watakaohusika katika uandikishaji daftari la wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaoanza Oktoba 11 hadi 20, 2024, kuepuka vikwazo kama kuruhusu misururu mirefu inayoweza kukatisha tamaa wananchi wanaojitokeza.

Ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi huo kwenye kata za Mwera na Mikunguni wilayani Pangani.

Ameyataja mazingira yanayokatisha tamaa kama vile kusimama kwenye misururu mirefu pasipo waandikishaji kuchukua hatua madhubuti za kuondokana na kadhia hizo, kunaweza kusababisha baadhi ya watu hasa wasiokuwa wavumilivu, kuondoka pasipo kujiandikisha.

Advertisement

“Ninawaagiza maafisa mtakaohusika na uandikishaji, epukeni kuwaweka watu kwenye foleni ndefu, tutapita kukagua na tutakayembaini anafanya uzembe, tutamuondoa,” amesema.

SOMA: Chalamila atoa maelekezo uchaguzi mitaa

Naye Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Wilaya ya Pangani, Ramadhan Hamad Rashid maarufu kama Diblo, amesema Watanzania wana imani kubwa na utashi wa Rais Samia, kufanikisha uchaguzi huo na Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa amani, utulivu na haki sawa.

Diblo amesema wananchi wa Pangani wana hulka na desturi za kuendeleza misingi ya amani na mshikamano katikati ya tofauti zao, na kwamba hakuna nafasi ya kuibuka vurugu zinazotokana na uchaguzi.

SOMA: Takukuru kutoa elimu ya rushwa uchaguzi mitaa