ETDCO kutekeleza mradi wa kuunganisha umeme Mbeya

MBEYA: MRADI wa kuunganisha umeme vitongoji 105 unaogharimu Sh bilioni 10.9 mkoani Mbeya utaanza kutekelezwa kupitia Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO).

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mradi huo katika kata ya Igawilo mkoani Mbeya, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema mradi huo utanufaisha wateja 3,465.

Spika Dk Tulia ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini alimshukuru Rais Samia Duluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wananchi kupitia miradi ya mbalimbali ya maendeleo.

Dk Tulia alisema tangu miradi ya REA kutekelezwa mwaka 2021/ 2022 serikali imetenga sh billioni 71 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijijini mkoani Mbeya.

Aidha Dk Tulia alimtakawa Mkandarasi wa mradi huo Kampuni ya ETDCO kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi wa vitongoji hivyo 105 wanufaike na nishati hiyo ya umeme.

“Nchi yetu ina umeme wa kutosha kutokana na mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, hivyo mradi huu wa usambazaji wa umeme kwenye vitongoji 105 unatakiwa kutelezwa kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na nishati hii ya umeme”, alisema Spika Dk.Tulia.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka ETDCO, Dismas Massawe, alisema kampuni hiyo iko tayari kutekeleza mradi huo kwa weledi na kwa wakati kama ilivyoanishwa kwenye mkataba ili wananchi hao waweze kupata nishati ya umeme kwa wakati uliopagwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, aliwataka wananchi wa Mbeya kujitayarisha kwa kuweka miundombinu ya kupokea huduma ya umeme katika makazi yao ili waweze kunufaika ipasavyo na mradi huo.

Wananchi wa Mkoa wa Mbeya wameipongeza serikali kwa mradi huo, huku wakisema utaongeza fursa za kiuchumi kupitia shughuli zinazohitaji umeme ikiwemo biashara ndogo ndogo, kilimo cha kisasa na usindikaji wa mazao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button