Ewura yataka taarifa sahihi kwa walaji

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Modestus Lumato

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Modestus Lumato, amezitaka Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini kuhakikisha zinatoa taarifa sahihi za huduma ya maji na usafi wa mazingira kwa wananchi ili kushamirisha upatikanaji wa huduma endelevu kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Lumato ametoa maelekezo hayo jana  jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha watendaji wa Mamlaka za Maji za Mikoa na Miradi ya Kitaifa kilicholenga kuhakiki taarifa za utendaji wa mamlaka hizo kwa mwaka 2021/22.

Lumato ameeleza kuwa tathmini iliyofanywa na Ewura imebaini kuwapo mamlaka za maji ambazo zimeendelea kuwasilisha taarifa zenye mapungufu kwenye kukidhi viwango vya huduma.

Advertisement

Pia uchakavu, ufanisi wa makusanyo wa maduhuli, muda wa upatikanaji wa huduma, ubora wa maji pamoja na idadi ya wananchi wanaopata huduma, hali hii inakwamisha kufanya tathmini ya hali halisi ya utendaji na upatikanaji huduma.

Naye Adam Ishara, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga ametaka kila mamlaka ya maji kujitahidi kutekeleza wajibu wake ikiwamo kuwa na takwimu sahihi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa huku akisisitiza kuwa, Wizara ipo tayari kutoa miongozo na ushirikiano unaohitajika muda wowote.

Kaimu Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira ambaye ni Meneja Ufundi wa Maji na Usafi wa Mazingira Ewura, Titus Safari ameeleza kuwa mchakato wa maandalizi ya ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji ni shirikishi hivyo kila mamlaka itumie kikao hicho kuthibitisha usahihi wa taarifa zake.

Watendaji kutoka mamlaka 25 za Majisafi na Usafi wa Mazingira za miji mikuu ya mikoa na mamlaka saba za miradi ya kitaifa wamehudhuria kikao kazi hicho kinachofanyika makao makuu ya Ewura jijini Dodoma.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *