Fahamu madhara ya vipodozi kwa wanaume

MATUMIZI ya mara kwa mara ya vipodozi kwenye saluni yana athari katika ngozi ikiwa ni pamoja na kusababisha kuota mvi katika umri mdogo.

Pia yanasababisha mzio wa ngozi pamoja na matatizo kwenye mfumo wa upumuaji kutokana na mwitikio hasi wa mwili dhidi ya baadhi ya viambato husika, HabariLEO limebaini.

Uchunguzi uliofanywa na HabariLEO umebaini kuwa vijana wengi wenye umri wa kuanzia miaka 30 hadi 40 wenye mvi nyingi kidevuni zimesababishwa na matumizi makubwa ya vipodozi wakati wa kunyoa ndevu kwenye saluni.

Wadau wa afya ya ngozi wamesema matumizi ya vipodozi pamoja na unyoaji wa ndevu mara kwa mara umesababisha vijana wengi kuwa na mvi za mapema hususani kidevuni ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo mvi zilionekana ni za watu wazima.

Baadhi ya vipodozi vilivyofanyiwa uchunguzi katika saluni za kiume ni pamoja na Aftershave, Super magic, Super black, Facial mask, Scrub, poda na spiriti kwa kuwa vinatengenezwa kwa kutumia kemikali mbalimbali zikiwemo za asili na viwandani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Athuman Ngenya alisema kama zilivyo bidhaa zingine za kikemikali, vipodozi vinaweza kusababisha athari mbalimbali kwa watumiaji kutokana na viambato vilivyotumika pamoja na matumizi yasiyo sahihi.

Alisema viambato hivyo vinaweza kusababisha athari za muda mfupi au mrefu kwa mtumiaji na kuongeza kuwa tafiti mbalimbali zimefanyika kuhusu athari za viambato vya vipodozi na matokeo yake ni kuzuiwa au kuruhusiwa kwa masharti kutokana na athari zake kwa umma.

“Miongoni mwa athari zinazoweza kusababishwa na matumizi ya vipodozi vya saluni ni ngozi kupoteza rangi yake, mzio wa ngozi, muwasho wa ngozi au kwenye mfumo wa hewa, ukavu wa ngozi unaosababisha ngozi kuwa dhaifu dhidi ya maambukizi na vipele vya ngozi,” alisema Dk Ngenya.

Mtaalamu wa magonjwa ya ngozi kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group, Dk Claud Mango alisema madhara ya ngozi kupoteza rangi yake ya asili kama alivyosema Dk Ngenya husababisha pia nywele zake kubadili rangi na kuwa nyeupe au mvi.

Dk Mango aliongeza kuwa baadhi ya vipodozi hivyo vina kiambata kinachoitwa hydroquinone ambacho kina uwezo mkubwa wa kuleta madhara kwenye ngozi wakati wa matumizi.

Katika kujiweka nadhifu na kuwa watanashati, vijana wengi wamekuwa wakitumia saluni kujiremba kwa vipodozi mbalimbali kama Super Magic, Super black, scrub, facial musk na hair bleach hali iliyotajwa kuwa chanzo cha mvi.

“Vipodozi vingi sana vina hiyo dawa ya hydroquinone ambayo kazi yake ni kukoboa ngozi, kutoka katika uasili wake na kuwa mpya. Kwa hiyo ngozi ikikobolewa usitarajie kuota nywele nyeusi,” alisema Dk Mango.

Alisema kwa kawaida katika mwili wa binadamu nywele nyeupe au mvi husababishwa na sumu ambazo mwili unazibakiza katika maisha ya mwanadamu na zinajikusanya taratibu na kuwa nyingi kupita kiasi.

Alisema chanzo cha sumu hiyo katika mwili wa mwanadamu ni kutokana na vitu mbalimbali anavyokutana navyo katika mazingira yake kama vyakula anavyokula, kemikali anazokutana nazo na kudhuru mwili, kazi anayofanya, msongo wa mawazo na ajali zinazosababisha ngozi kuathirika.

“Hizi sumu zinakwenda kuharibu seli zinazotengeneza rangi nyeusi kwenye ngozi hali inayosababisha nywele kubadili rangi na kuwa nyeupe.

“Nywele zinazoanza kuchakaa ndizo zinazoathiriwa mapema na sumu hiyo ambazo ni za kidevuni na za kuzunguka usawa wa masikio,” aliongeza Dk Mango.

Ofisa Utafiti Mwandamizi Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Maria Ngilisho alisema mambo yanayosababisha mvi katika umri wa mapema ni kuchoka kwa seli zinazotengeneza rangi nyeusi ya ngozi na nywele.

Aliongeza kuwa msongo wa mawazo, mfumo wa kinga wa mwili kushambulia seli zingine, uvutaji wa sigara, upunguvu wa virutubisho mwilini na mvi za kuruithi ni baadhi ya mambo mengine yanayosababisha mtu kuota mvi mapema.

Mhudumu wa saluni ya Fuga iliyopo katika Mataa wa Kinyonga, Mji Mpya mkoani Dodoma anayejulikana kwa jina maarufu la Man Fuga aliliambia HabariLEO kuwa katika uzoefu wake wa miaka 30 ya kunyoa, mvi zinazowaota vijana kidevuni zinasababishwa na matumizi makubwa ya vipozozi hususani vya Super Magic na Super black.

Mtafiti Mwandamizi wa masuala ya afya anayefanyia kazi zake katika Mkoa wa Mwanza, Ernest Sebarua ambaye ni mwathiriwa wa mvi za mapema kidevuni alisema katika kazi zake alipata maelezo kutoka kwa mtaalamu mmoja kuwa sehemu ya mwisho ya shina la nywele zote mwilini ni nyeupe hivyo kadiri nywele zinavyokatwa zinasababisha ile sehemu nyeupe kujongea kwenda nje.

“Kadri unavyokata nywele ndivyo ile sehemu nyeupe inajongea kwenda nje, ndio maana sehemu ambazo nywele hukatwa sana huanza kuwa na mvi mapema ambazo ni kidevuni na katika paji la uso, hivyo vijana wananyoa ndevu mara nyingi kuliko kichwani,” aliongeza.

Kinyozi Omari, Ally Badi anayefanya shughuli zake Kata ya Magole Tarafa ya Kitunda, Dar es Salaam alisema vijana wanaotumia Super black wako katika hatari kubwa ya kuota mvi katika umri mdogo zaidi.

Alisema sababu nyingine ya mvi za mapema ni kunyoa mara kwa mara huku akiongeza kuwa matumizi ya spiriti yanakomaza kidevu hali inayomfanya kijana wa miaka 20 kuonekana kama wa miaka 40.

Jacob Pangani anayefanya kazi ya kunyoa katika saluni ya Mussa iliyopo Kwa Mpemba katika Kata ya Magole alisema wateja wengi wanaokuja kwake wamekataa kutumia After Shave pamoja na spiriti kwa kuwa inawaotesha mvi kwa kasi na badala yake kuamua kutumia poda.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button